Dirisha la Uhamisho EPL lafungwa; Zifahamu biashara zilizofanyika siku ya mwisho

Dirisha la uhamisho katika ligi kuu Uingereza (EPL) lilifungwa mnamo saa sita usiku wa Agosti 31 na biashara kadhaa ziliendelea siku ya mwisho.

Christiano Ronaldo, Takehiro Tomoyasu na Saul Niguez
Christiano Ronaldo, Takehiro Tomoyasu na Saul Niguez
Image: HISANI

Dirisha la uhamisho katika ligi kuu Uingereza (EPL) lilifungwa mnamo saa sita usiku wa Agosti 31  na biashara kadhaa ziliendelea siku ya mwisho.

Klabu ya Manchester United ilitangaza kukamilisha usajili wa mshambulizi matata Christiano Ronaldo aliyetia saini mkataba wa miaka miwili na uwezekano wa nyongeza ya mwaka mwingine mmoja.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 alirejea Old Trafford baada ya kuondoka miaka 12 iliyopita na kujiunga na Real Madrid ya Uhispania.

Klabu hiyo hata hivyo ilimuuza mshambulizi Daniel James kwa klabu ya Leeds United kwa pauni milioni 25.

Raia huyo wa Wales mwenye umri wa miaka 23 alitia saini mkataba wa miaka mitano na Leeds.

Klabu ya Arsenal ambayo imeandikisha matokeo hafifu tangu msimu wa EPL 2021/22 uanze iliongeza huduma za mlinzi Takehiro Tomoyasu aliyenunuliwa kutoka Bologna kwa pauni milioni 16.

Raia huyo wa Ujapani mwenye umri wa miaka 22 alitia saini mkataba wa miaka mingi na Wanabunduki na atavalia jezi nambari 18.

Arsenal ilimuuza mlinzi Hector Bellerin kwa klabu ya Real Betis kwa mkopo. Mlinda lango Alex Runarsson pia alijiunga na OH Leuven kwa mkopo.

Mshambulizi Reis Nelson ni mchezaji mwingine ambaye aliondoka Emirates na kujiunga na Feyenoord ya  Uholanzi kwa  mkopo.

Klabu ya Chelsea ilipata huduma za kiungo Saul Niguez kutoka Atletico Madrid kwa mkopo wa msimu mmoja.

Tottenham ilisajili mlinzi Emerson Loyal kutoka Barcelona. Loyal alitia saini mkataba wa miaka mitano na Tottenham na atavalia jezi nambari 18.

Mlinzi Serge Aurier kutoka Ivory Coast hata hivyo aliondoka Tottenham baada ya makubaliano ya pande zote kukatiza mkataba wake na klabu hiyo ya London.