Kocha Mkuu wa Harambee Stars Ghost Mulee ajiuzulu

Muhtasari

Kocha Mkuu wa Harambee Stars Ghost Mulee ajiuzulu

Ghost Mulee
Image: Maktaba

Kocha mkuu wa timu ya kitaifa Jacob Ghost Mulee na timu yake yote ya ufundi wamejiuzulu kutoka Harambee Stars kwa idhini ya pamoja baada ya kuwajibika kwa miezi kumi na moja.

Mulee aliteuliwa kama mkufunzi mkuu wa timu hiyo kwa mara ya kumi na mbili mnamo Oktoba 20, 2020, akichukua nafasi ya mtangulizi wake Francis Kimanzi.

Shirikisho la Soka la Kenya FKF limesema katika taarifa yake Jumatano kwamba Mulee, Msaidizi wake Twahir Muhidin, na Kocha wa Walinda mlango Haggai Azande walikubaliana kujiuzulu.

Shirikisho hilo lilisema kwamba makocha wasaidizi Ken Odhiambo, na William Muluya watabaki kwenye timu hiyo kwani inafanya kazi kujenga benchi la ufundi la Harambee Stars.

"FKF inamshukuru sana Kocha Mulee na wafanyikazi wake wanaoondoka kwa huduma yao ya kujitolea na kazi. Shirikisho linawatakia kila la kheri katika juhudi zao za baadaye, "katibu mkuu wa FKF Barry Otieno alisema.

Aliongeza kuwa utaftaji wa kocha mkuu wa timu ya kitaifa tayari unaendelea na tangazo litatolewa hivi karibuni.