Matokeo ya mechi za ufunguzi wa ligi ya mabingwa Ulaya msimu wa 2021/22

Muhtasari

•Mashetani wekundu walionyeshwa kivumbi na wenyeji wao Young Boys kwa kucharazwa mabao mawili kwa moja.

•Washindi wa kombe hilo msimu uliopita Chelsea walianza hatua ya kulinda taji huku wakipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Zenit ya Urusi

Image: TWITTER//YOUNG BOYS

Hatimaye  msimu wa 2021/22 wa ligi ya mabingwa uling'oa nanga usiku wa Jumanne huku mechi nane zikichezwa katika nyanja mbalimbali bara Ulaya.

Michuano hiyo ilianza na mechi kati ya Young Boys na Manchester United huku Sevilla wakicheza dhidi ya Salzburg mida ya saa mbili kasorobo. 

Mashetani wekundu walionyeshwa kivumbi na wenyeji wao Young Boys kwa kucharazwa mabao mawili kwa moja.

Mshambulizi matata Christiano Ronaldo alikuwa wa kwanza kutikisa wavu katika dakika ya 13 ila nguvu za United zikaanza kufifia baada ya beki Aaron Wan-Bissaka kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 35. Mabao mawili ya Young Boys yalifungwa na Nicolas Ngamaleu na Jordan Siebatcheu katika kipindi cha pili.

Mechi katika ya Sevilla na Salzburg iliishia sare ya moja kwa moja baada ya Luka Sucic na Ivan Rakitic kufungia Salzburg na Sevilla mtawalia katika kipindi cha kwanza.

Mechi sita zilichezwa mida ya saa nne usiku mchuano mkubwa ukiwa kati ya Barcelona na Bayern Munich.

Barcelona walionyeshwa kivumbi nyumbani baada ya miamba wa soka Ujerumani kuwacharaza mabao matatu bila jawabu. Washambulizi Thomas Muller na Robert Lewandoski walisaidia Bayern kupata ushindi huo mkubwa.

Washindi wa kombe hilo msimu uliopita Chelsea walianza hatua ya kulinda taji huku wakipata ushindi wa 1-0 dhidi ya Zenit ya Urusi. Mshambulizi Romelu Lukaku ndiye alifungia Chelsea bao la pekee la mechi hiyo.

Juventus walipata ushindi wa 3-0 ugenini dhidi ya Malmo FF. Alex Sandro, Paul Dybala na Alvaro Morata walifungia Juve.

Villareal walitoka sare ya 2-2 na Atlanta huku mechi kati ya Dynamo Kiev na Benfica  pamoja na Lille dhidi ya Wolfsburg ziliashia sare ya sufuri kwa sufuri.