Heko! Michael Olunga afungia klabu yake mabao 5 ndani ya dakika 30 punde baada ya kupona jeraha

Muhtasari

•Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 aliwaacha wengi vinywa wazi baada ya kufungia klabu yake ya Al-Duhail mabao matano kwenye mechi yake ya kwanza baada ya kupona jeraha.

•Kwa sasa klabu ya Olunga ya Al-Duhail iko katika nafasi ya pili na pointi 12 huku Olunga aliwa anaongoza jedwali la wafungaji bora akiwa amefunga jumla ya mabao 7.

Image: TWITTER// AL DUHAIL

Mshambulizi matata wa Harambee Stars Michael Olunga ameendelea kuonyesha dunia nzima umahiri wake katika mchezo wa soka kila uchao.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 aliwaacha wengi vinywa wazi baada ya kufungia klabu yake ya Al-Duhail mabao matano kwenye mechi yake ya kwanza punde baada ya kupona jeraha.

Olunga alisaidia Al-Duhail kupata ushindi mkubwa wa 5-0 dhidi ya Al Sailiya siku ya Jumapili baada ya kufunga mabao yote matano katika kipindi cha pili.

Olunga aliingia kama mchezaji wa akiba katika dakika ya 45, wakati ambapo hakuna aliyekuwa ametingisha wavu wa mwingine kati ya timu hizo mbili za Qatar.

Bao la kwanza la Olunga liliingia wavuni katika dakika ya 56 kisha akafunga lingine baada ya dakika sita. Mabao yaliendelea kumiminika kutoka kwa buti la gwiji huyo wa soka huku akiendelea kufunga katika dakika ya 68, 79 na 85.

Kwa sasa klabu ya Olunga ya Al-Duhail iko katika nafasi ya pili na pointi 12 huku Olunga aliwa anaongoza jedwali la wafungaji bora akiwa amefunga jumla ya mabao 7.