EPL 2021/22: Matokeo ya raundi ya 8, Hali ilivyo kwenye jedwali

Michuano hiyo iliingia katika raundi ya nane siku ya Jumamosi

Muhtasari

•Mashetani wekundu walinyolewa kichwa bila maji na wenyeji wao Leicester ambao waliwanyuka mabao 4-2 na kupunguza kasi yao ya kuwania kombe la msimu hu

•Kwa sasa Chelsea inaongoza jedwali na pointi 19, Liverpool  ya pili na pointi 18, City inafuata na pointi 17 huku Brighton ikifunga nne bora na pointi 15.

•Mohammed Salah wa Liverpool (7) , Jamie Vardy wa Leicester (7) na Michail Antonio  wa Westham (5) wanaongoza kwa ufungaji mabao.

Image: FACEBOOK// MANCHESTER UNITED

Wikendi iliyotamatika mashindano ya kandanda ambayo yanatazamwa zaidi duniani ya EPL yaliweza kurejea  baada ya kipindi cha wiki mbili cha mapumziko ya kimataifa.

Michuano hiyo iliingia katika raundi ya nane siku ya Jumamosi huku mechi ya ufunguzi ikiwa kati ya Watford na washindi wa kombe la EPL msimu wa 2019/20 Liverpool ambayo ilichezwa mida ya saa nane unusu alasiri.

Vijana wa Klopp walionyesha wenyeji wao kivumbi ugani Vicarage Road kwa kuwalaza mabao matano bila jawabu. Roberto Firmino (3), Sadio Mane na Mohammed Salah ndio walifungia Liverpool na kuwawezessha kupata ushindi huo mkubwa.

Jumla ya mechi tano zilichezwa saa kumi na moja jioni.

Mechi ya kusisimua zaidi ilikuwa kati ya Leicester na Manchester United ambayo ilichezewa ugani King Power.

Mashetani wekundu walinyolewa kichwa bila maji na wenyeji wao Leicester ambao waliwanyuka mabao 4-2 na kupunguza kasi yao ya kuwania kombe la msimu huu. Mabao ya Leicester yalifungwa na Youri Tielemans. Caglar Soyuncu, Jamie Vardy  na Patson Daka huku washambulizi Mason Greenwood na Marcus Rashford wakifungia United mabao mawili ya kufutia machozi.

Mechi nyingine ilikuwa kati ya washindi wa EPL 2020/21 Manchester City na Burnley. Bernardo Silva na Kevin De Bruyne walifungia City na kuwawezesha kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji wao.

Aston Villa walipoteza 2-3 nyumbani dhidi ya Wolves, Southampton wakawabwaga chini Leeds 1-0 hukumechi kati ya Norwich na Brighton ikiisha sare tasa.

Mechi ya mwisho siku ya Jumamosi ilikuwa kati ya Brentford na Chelsea ambayo ilichezwa saa moja unusu usiku ugani Brentford Community Stadium.

Vijana wa Tuchel walipata ushindi wa 1-0, beki Ben Chilwell akifunga bao la pekee la mechi hiyo katika dakika ya 45 na kuwasukuma hadi nafassi ya kwanza.

Mechi mbili tu zilichezwa siku ya Ijumaa.

Image: INSTAGRAM// PREMIER LEAGUE

Everton waliwakaribisha Westham ugani Goodison Park mida ya saa kumi alasiri ila wakashindwa kuwika nyumbani na kupoteza 0-1. Beki Angelo Ogbonna alifungia Westham bao la pekee la mechi.

Tottenham walikuwa wageni wa Newcastle ugani St James Park mida ya saa kumi na mbili jioni na wakaweza kunyamazisha wenyeji wao kwa mabao 3-2.

Mechi iliyosalia kati ya  Arsenal na Crystal Palace inatarajiwa kuchezwa mida ya saa nne usiku wa Jumatatu ugani Emirates.

Kwa sasa Chelsea inaongoza jedwali na pointi 19, Liverpool  ya pili na pointi 18, City inafuata na pointi 17 huku Brighton ikifunga nne bora na pointi 15.

Nafasi tatu za mwisho zinakaliwa na Burnley, Newcastle na Norwich ambazo ziko na pointi 3,3 na 2 mtawalia.

Mohammed Salah wa Liverpool (7) , Jamie Vardy wa Leicester (7) na Michail Antonio  wa Westham (5) wanaongoza kwa ufungaji mabao.