Wanabunduki washindwa kuwika nyumbani dhidi ya Palace kwa mara ya nne mfululizo, 2-2

Muhtasari

•Mara ya mwisho kwa klabu ya Arsenali kupata ushindi dhidi ya Palace ugani Emirates ilikuwa mwezi Januari mwaka wa 2018 ambapo walishinda 4-1.

•Matokeo hayo yaliacha Arsenal katika nafasi ya 12 na pointi 11 huku vijana wa Patrick Viera wakikalia nafasi ya 14 na pointi 8.

Image: INSTAGRAM// ARSENAL

Wanabunduki waliweza kudhibitiwa nyumbani na majirani wao Crystal Palace kwa mara nne mfululizo usiku wa Jumatatu.

Mechi ya raundi ya nane kati ya timu hizo mbili za London ambayo ilichezwa mida ya sa nne usiku iliishia sare ya 2-2.

Mara ya mwisho kwa klabu ya Arsenali kupata ushindi dhidi ya Palace ugani Emirates ilikuwa mwezi Januari mwaka wa 2018 ambapo walishinda 4-1.

Vijana wa Arteta walitangulia kwa kufunga katika mechi iliyochezwa usiku wa Jumatatu.

Bao la mshambulizi matata Pierre-Emerick Aubameyang katika dakika ya nane liliwapa wanabunduki uongozi hadi dakika ya 50 ambapo Mbeligiji Christian Benteke alisawazishia Palace.

Dakika 23 baadae mshambulizi Odsonne Edouard alifungia Palace bao la pili na kuangamiza matumaini ya Arsenal ya kupata ushindi. 

Mechi hiyo ilikuwa imeonekana kama kwamba ingekamilika hivo kwani dakika 90 za kawaida zilitamatika kama Palace ingali inaongoza 1-2. Hata hivyo mshambulizi Alexandre Lacazette aliweza kufungia klabu yake bao la kuficha aibu katika dakika ya 90+5.

Matokeo hayo yaliacha Arsenal katika nafasi ya 12 na pointi 11 huku vijana wa Patrick Viera wakikalia nafasi ya 14 na pointi 8.