Barca yampiga kalamu kocha Ronald Koeman, Xavi apendekezwa kuchukua wadhifa huo

Muhtasari

•Rais wa Barcelona Joan Laporta alifahamisha Koeman kuhusu uamuzi wa bodi wa kumuachisha kazi punde baada ya miamba hao wa soka nchini Uhispania kupoteza ugenini dhidi ya Rayo Vallecano.

•Inasemekana kwamba Barca iko tayari kulipa fedha zinazodaiwa na Al Sadd kusitisha mkataba wake na Xavi ili aruhusiwe kuondoka na kujiunga na klabu yake ya zamani kama kocha.

Image: HISANI

Ni rasmi kwamba klabu ya Barcelona imemfuta kazi kocha wake Ronald Koeman ambaye amekuwa akishikilia wadhifa huo kwa kipindi cha miezi 14.

Barca ilitangaza habari kuhusu kufutwa kwa raia huyo wa Uholanzi kupitia tovuti rasmi ya klabu usiku wa Jumatano.

Koeman alipigwa kalamu kufuatia mwanzo mbaya katika kombe la LALIGA msimu wa 2021/22 .

Rais wa Barcelona Joan Laporta alifahamisha Koeman kuhusu uamuzi wa bodi wa kumuachisha kazi punde baada ya miamba hao wa soka nchini Uhispania kupoteza ugenini dhidi ya Rayo Vallecano.

Kocha  huyo mwenye umri wa miaka 58 anatarajiwa kuaga wachezaji kwaheri siku ya Alhamisi uwanja wa mazoezi wa Ciutat Esportiva.

"FC Barcelona ingependa kumshukuru Koeman kwa kazi huduma aliyotoa kwa klabu na kumtakia mazuri katika taaluma yake" Klabu ya Barcelona ilitangaza.

Kwa sasa Barca inashikilia nafasi ya 9 baada ya kunyakua pointi 15 tu kutoka kwa mechi 10 za LALIGA 2021/22 ambazo zimeweza kuchezwa tayari.

Bingwa wa klabu hiyo Xavi ambaye kwa sasa ni kocha wa klabu ya  Al Sadd iliyo Qatari ni mmoja wa wanaopendekezwa sana kuchukua nafasi ya Koeman.

Inasemekana kwamba Barca iko tayari kulipa fedha zinazodaiwa na Al Sadd kusitisha mkataba wake na Xavi ili aruhusiwe kuondoka na kujiunga na klabu yake ya zamani kama kocha.