Kombe la dunia 2022: Timu gani zimeshafuzu mpaka sasa na zipi zenye matumaini?

Muhtasari

•Kwa timu zitakazosafiri kujulikana wiki hii, zile zitakazofungasha virago na zile zilizo kwenye hati hati, mguu ndani mguu nje zinajulikana pia.

Image: GETTY IMAGES

Safari ya kwenda Qatar 2022 kwa ajili ya fainali za kombe la dunia inakaribia kabisa, kwa timu zitakazosafiri kujulikana wiki hii, zile zitakazofungasha virago na zile zilizo kwenye hati hati, mguu ndani mguu nje zinajulikana pia.

Kwa upande wa Ulaya, washindi 10 wa makundi wanakwenda moja kwa moja kwenye fainali hizo, ambazo zitapigwa kati ya Novemba 21 na Disemba 18, 2022.

Mashidano ya Qatar yatakuwa ya mwisho kushirikisha timu 32, kwa sababu idadi ya timu zimeongezwa mpaka 48 kuanzia fainali za mwaka 2026 zitakazofayika katika nchi za Marekani, Mexico na Canada.

Qatar, itashiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa, NA imefuzu kama mwenyeji, ikitarajiwa kuwa timu ya kawaida katika fainali hizo.

UEFA: ULaya

Bara la Ulaya litawakilishwa na timu 13, timu 10 zilizoongoza hatua ya makundi zimefuzu moja kwa moja, na nafasi 3 zilizosalia zitashindaniwa na timu 10 zilizoshika nafasi ya pili kwenye makundi na timu mbili zilizoshika nafasi ya tatu au chini kutoka mashindao ya Nations League ya Ulaya.

1: Ujerumani

Bingwa mara 4 wa kombe la dunia, Ujerumani ilikuwa timu ya kwanza kufuzu fainali za 2022, ikiichabanga Macedonia 4-0 , ilikuwa Oktoba 11 na kujihakikishia nafasi ya kwanza ya kufuzu kutoka kundi J.

2: Ufaransa

Image: GETTY IMAGES

Mabingwa watetezi nao wamefuzu kupitia Ulaya, Kylian Mbappé alifunga mabao 4 Ufaransa ikiigaragaza Kazakhstan 8-0 na kuisaidia timu hiyo kuongoza kundi D na kuiacha Finland iiyokuwa inaikaribia kwneye nafasi ya pili.

3: Ubelgiji

Ubelgiji ambao walishika nafasi ya 3 katika kombe la dunia mwaka 2018, nao wanaenda Qatar, baada ya Jumamosi kushinda 3-1 dhidi ya Estonia na kujihakikishia nafasi ya juu kutoka kundi E.

4: Croatia

Walishika nafasi ya pili mwaka 2018. Croatia wamefuzu kwa ubabe kutoka kundi H siku ya Jumamosi. Ilikutana na Urusi, iliyokuwa inataka alama moja tu kufuzu, lakini vijana wa Zlatko Dalic wakalazimisha sare, kwa goli la dakika 81 la kujifunga la Fedor Kudryashov lililoipeleka Urusi kwenye mtoano.

5: Hispania

Alvaro Morata
Alvaro Morata
Image: GETTY IMAGES

Jumapili Hispania imefuzu fainali zake za 12 mfululizo kutoka kundi B, ikiipiga kumbo Sweden kileleni mwa kundi lake huko Seville. Mabingwa hao wa kombe la dunia wa mwaka 2010 walihitaji sare tu kufuzu moja kwa moja, lakini goli la Álvaro Morata lilitosha kuipeleka Hispania kwenye fainali za Qatar.

6: Serbia

Katika mchezo kudi Aulioshangaza, Serbia imeinyuka 2-1 Ureno nyumbani kwake iliyokuwa na Cristiano Ronaldo na kufuzu moja kwa moja, goli la dakika ya mwisho la Aleksandar Mitrovic limeikata maini Ureno.

Ronaldo atasubiri mpaka mwezi Machi mwakani, kujua kama watafuzu ama la.

7: Switzerland

Switzerland imeichapa Bulgaria 4-0 na kufuzu fainali za mwakani kwa kumaliza kileleni kwenye kundi C baada ya Ireland Kaskazini kuilazimisha sare ya 0-0 Italia huko Belfast.

Kikosi cha Roberto Mancini, kitapaswa kusubiri mpaka mwezi Machi kufuzu kombe la dunia kupitia mchujo

8: England

Image: GETTY IMAGES

England imefuzu kombe la dunia baada ya kuizaba San Marino, 10-0 timu inayoburuza mkia kwenye viwango vya soka duniani. Kikosi cha Gareth Southgate kinapewa nafasi kubwa kushinda kombe la dunia mwaka ujao, baada ya kufika nusu fainali katika mashindao yaliyopita ya Urusi na ikaingia fainali katika mashindano ya Euro 2020 katika majira ya joto.

England imefunga magoli 10 tangu mwaka 1964, Harry Kane akifunga mabao 4 ndani ya dakika 15, Emily Smith akianza kwa mara ya kwanza na kufunga bao moja na kutengeneza bao moja.

9: Denmark

Denmark ilikuwa taifa la pili kufuzu kombe la dunia mwakani huko Qatar baada ya ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Austria ikiendeleza rekodi yake nzuri ya ushindi kwenye kundi F.

Leo Jumanne, Uholanzi yenye alama 20, Uturuki na Norway (zote zikiwa na alama 18 points) mojawapo inaweza kufuzu kutoka kundi G na kukamilisha timu 10 kutoka Ulaya. Uholanzi inakutana na Norway, Uturuki inakutana na Montenegro.

Timu gani zingine zimefuzu kombe la dunia mwezi huu?

CONMEBOL: Amerika Kusini

Amerika ya Kusini wana nafasi nne za moja kwa moja na 3 kutoka Amerika Kaskazini, huku nafasi iliyosalia itawaniwa na timu kutoka mabara hayo mawili. Mabingwa mara mbili wa kombe la dunia, Argentina itakuwa timu ya pili kufuzu kutoka kanda ya CONMEBOL kufuzu fainali za Qatar 2022 kama itaifunga Brazil huko San Juan leo. Sare itatosha kwa vijana wa Lionel Scaloni kufuzu kama Chile na Colombia zitapoteza michezo yao.

AFC: Asia

Bara la Asia kuna nafasi 4, ipo nafasi moja ambayo ama timu kutoka Asia ama Oceania itafuzu. Hakuna timu iliyofuzu kutoka Asia, mpaka sasa makundi mawili ya timu sita sita yanaendelea na michezo, huku Iran, Korea Kusini, Saudi Arabia na Australia wakionekana kufanya vizuri na dalili njema za kufuzu.

CAF: Afrika

DRC Congo wakishangilia moja ya mabao yao kwa mtindo wao maarufu wa 'kuchapa fimbo'
DRC Congo wakishangilia moja ya mabao yao kwa mtindo wao maarufu wa 'kuchapa fimbo'
Image: GETTY IMAGES

Timu 5 za kuwakilisha bara la Afrika kwenye kombe la dunia mwakani hazijafahamika, mpaka kuchezwa kwa raundi ya 3 na ya mwisho mwezi Machi. Mpaka sasa mataifa 6 ya DR Congo, Ghana, Mali, Misri, Senegal na Misri yameingia raundi ya mwisho.

CONCACAF: Amerika Kaskazini,kati, na Caribbean

Mpaka sasa Marekani, Mexico na Canada wanaonekana kufanya vizuri wakielekea njia ya Qatar, ingawa safari bado ndefu, zimesalia michezo saba.