PSG imezindua rasmi kituo cha kufundishia soka kwa vijana nchini Rwanda

Muhtasari
  • PSG imezindua rasmi kituo cha kufundishia soka kwa vijana nchini Rwanda
Image: BBC

Mabingwa wa Ufaransa,timu ya Paris Saint Germain imezindua rasmi kituo cha kufundishia soka kwa vijana nchini Rwanda, ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya miaka 3 ya kibiashara na kuinua sekta ya utalii nchini Rwanda.

Uzinduzi rasmi wa Shule ya kufundishia Soka ya PSG nchini Rwanda umefanyika katika mji wa Huye kuliko makao makuu ya shule hiyo.

Bi Nadia Benmokhtar, mkurugenzi mkuu wa shule za soka za PSG, alisema kuwa shule ya PSG huko Huye kwa namna ya pekee inafundisha watoto mpira wa miguu bila kulipa gharama yoyote tofauti na sehemu nyingine duniani ambako timu hiyo ina shule za kufundishia soka.

Paris Saint Germain ina shule 122 duniani zinazofundisha watoto mpira wa miguu.Alisema sababu iliyoifanya PSG kuchagua kufungua shule yake mjini Huye ni kwa vile ni jiji lenye shule nyingi hali inayorahisisha kuchagua watoto wenye vipaji.

"Tulituma timu ya wataalamu waliofanya kazi na Serikali ya Rwanda kuchagua mahali pa kuweka shule yetu. Hapa Huye tumegundua kuna shule na vyuo vikuu vingi ambavyo vinarahisisha kuchagua watoto wenye vipaji katika soka, ni mahali pa michezo,soka ikiwa maarufu sana."

Nadia anasema PSG na Rwanda zitanufaika na mradi wa shule hiyo ya kufundisha soka watoto.

"Kadiri mradi unavyokua, tutatoa ajira zaidi kwa Wanyarwanda kwa sababu mmeona makocha na wakuu wa shule ni Wanyarwanda, na ndivyo itakavyokuwa," alisema watoto wa soka ni Wanyarwanda.

"Siwezi kusema kwamba watoto hawa wataichezea PSG kwa sababu ni timu ipo kwenye kiwango cha juu, inawezekana labda mmoja anaweza kujitokeza na kwenda kucheza Ufaransa, lakini haijakusudiwa, bali Rwanda na timu za Rwanda zinaweza kupata wachezaji bora walioandaliwa vizuri na wenye viwango bora''

Watoto wenye umri kati ya miaka 6 na 14 wapo katika hatua tofauti za kucheza soka.

Kwa hatua ya mwanzo Kituo cha soka cha PSG kina watoto 172 wakiwemo wavulana 110 na wasichana 72.

Bwana Theonas Ndungutse, mwalimu mkuu wa shule ya PSG nchini Rwanda, aliambia BBC kuwa watoto hao wanasomea katika shule mbali mbali za mji wa Huye na kisha baada ya masomo yao ya kawaida hufundishwa kusakata kabumbu lakini kwamba kadri mradi utakavyopanuka watafikiri kujenga kuwaweka katika mabweni.

Shule hiyo ni sehemu ya makubaliano ya ushirikiano baina ya Rwanda na timu ya PSG ya miaka 3 yaliyotiwa saini mwaka 2019 .

Makubaliano hayo ya kibiashara yanalenga kuendeleza sekta ya utalii nchini Rwanda katika kampeni ya kuhamasisha watu kutembelea Rwanda ya 'Visit Rwanda'

Kadhalika "Bango lenye maneno 'Tembea Rwanda' linaonyeshwa katika uwanja wa Parc des Princes, kwenye fulana za timu ya wanawake ya Paris Saint-Germain pamoja na nyuma ya nguo zao za mazoezi za timu ya PSG.