Michael Carrick ajiuzulu na kugura United baada kuwazima Wanabunduki, 3-2

Muhtasari

•United ilitangaza kuhusu hatua hiyo ya Carrick punde baada ya kuandikisha ushindi wao wa kwanza wa EPL dhidi ya Arsenal tangu mwaka wa 2017 usiku wa Alhamisi.

•Alijiunga na  kikosi cha wakufunzi mwaka wa 2018 na alihudumu kama msaidizi wa meneja Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer.

Aliyekuwa kiungo na kocha wa muda wa United Michael Carrick
Aliyekuwa kiungo na kocha wa muda wa United Michael Carrick
Image: MANCHESTER UNITED

Michael Carrick (40) amefanya maamuzi ya kujiulu kutoka kwa wadhfa wake kama kocha wa timu ya kwanza ya United na kugura klabu hiyo kufuatia kutamatika kwa kipindi chake kama meneja wa muda.

United ilitangaza kuhusu hatua hiyo ya Carrick punde baada ya kuandikisha ushindi wao wa kwanza wa EPL dhidi ya Arsenal tangu mwaka wa 2017 usiku wa Alhamisi.

Katika mechi yake ya mwisho kusimamia, Carrick alishuhudia United ikicharaza wanabunduki 3-2 ugani Old Trafford.

Kiungo huyo wa zamani wa mashetani wekundu na timu ya taifa ya Uingereza almaarufu kama Three Lions anaondoka Old Trafford baada ya kusimamia klabu hiyo katika mechi tatu ambapo wameshinda mara mbili na kuandikisha sare moja.

Alijiunga na  kikosi cha wakufunzi mwaka wa 2018 na alihudumu kama msaidizi wa meneja Jose Mourinho na Ole Gunnar Solskjaer.

Alichezea klabu hiyo katika mechi 464 kati ya mwaka wa 2006 na 2018 akishinda ligi mara tano, Champions League na Europa mara moja moja.

Carrick alisema sasa ni wakati mwafaka kwake kuondoka United huku akiwashukuru wachezaji na wafanyikazi wenzake pale Old Trafford kwa ushirikiano mzuri.

Ralf Rangnick atajaza nafasi iliyokuwa imeshikiliwa na Carrick hadi mwisho wa msimu wa 2021/22  huku mechi yake ya kwanza kusimamia ikiwa dhidi ya Crystal Palace siku ya Jumapili.