Lukaku hana raha Chelsea, atamani kurudi Inter Milan

Muhtasari

•, Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikiri kwamba hafurahishwi na mfumo wa soka ambao kocha Thomas Tuchel anatumia.

•Amesema anajutia sana namna alivyoondoka  Serie A na jinsi alivyowaaga mashabiki wa Inter huku akisema angependa kurudi.

Mshambuliaji wa Chelsea Romelu Lukaku
Mshambuliaji wa Chelsea Romelu Lukaku
Image: HISANI

Mshambuliaji matata wa Chelsea Romelu Lukaku amekiri kwamba hajaridhishwa na jinsi mambo yanavyoendeshwa katika klabu hiyo ya London.

Akiwa kwenye mahojiano na Sky Sports, Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikiri kwamba hafurahishwi na mfumo wa soka ambao kocha Thomas Tuchel anatumia.

Lukaku ambaye alirejea Chelsea mwanzoni wa msimu wa 2021/22 kwa pauni 97.5M amesema yuko sawa kimwili lakini kisaikolojia hana furaha hata kidogo akiwa pale Stamford Bridge.

"Kimwili niko sawa. Lakini sifurahishwi na hali ilivyo Chelsea. Tuchel amechagua kucheza na mfumo mwingine - sitakata tamaa, nitakuwa mtaalamu. Sifurahishwi na hali hiyo lakini mimi ni mtaalamu - na siwezi kukata tamaa sasa" Lukaku alisema.

Kufuatia hali hiyo nyota huyo wa soka amekiri anatamani kurejea katika klabu yake ya zamani Inter Milan ya Italia.

Amesema anajutia sana namna alivyoondoka  Serie A na jinsi alivyowaaga mashabiki wa Inter huku akisema angependa kurudi.

"Sasa ni wakati mwafaka wa kueleza hisia zangu. Nimekuwa nikisema kila mara nina Inter moyoni mwangu: Najua nitarudi Inter, natumai hivyo. Ninaipenda Italia, huu ni wakati mwafaka wa kuzungumza na kuwafahamisha watu ni nini kilitokea.. Nadhani kila kitu kilichotokea msimu wa joto uliopita hakikupaswa kutokea hivi... jinsi nilivyoondoka Inter, jinsi nilivyoondoka kwenye klabu, jinsi nilivyowasiliana na mashabiki wa Inter - hii inanisumbua kwa sababu haukuwa wakati mwafaka" Alisema Lukaku.

Mshambuliaji huyo amecheza dakika chache mno tangu The Blues walipomsajili Thomas Tuchel kama kocha mpya.