EPL 2021/22: Matokeo ya raundi ya 21

Muhtasari

•Jumla ya mechi saba zilichezwa siku ya Jumamosi na Jumapili katika viwanja tofauti nchini Uingereza.

Image: LIVERPOOL

Kombe la EPL bado linaendelea kushika kasi huku  sasa tukiingia katika raundi ya 21 ya michuano wikendi iliyotamatika. 

Jumla ya mechi saba zilichezwa siku ya Jumamosi na Jumapili katika viwanja tofauti nchini Uingereza.

Mechi ya ufunguzi ilikuwa kati ya Arsenal na Manchester City ambayo ilichezwa Jumamosi mwendo wa saa tisa unusu alasiri ugani Emirates.

Wanabunduki walipoteza mechi hiyo katika dakika za lala salama baada ya kiungo Rodri kufungia City bao la pili na kufanikisha ushindi wa 1-2.

Arsenal ilitangulia kwa kufunga katika dakika ya 31 kupitia msambulizi Bukayo Saka. Vijana wa Pep Guardiola walisawaziha katika dakika ya 57 kupitia mkwaju wa penalti wa Riyad Mahrez. Mlinzi Gabriel Magalhaes alionyeshwa kadi nyekundu dakika mbili baadae na kupunguza makali ya vijana wa Mikel Arteta.

Watford waliwakaribisha Tottenham Hotspurs ugani Vicarage Road mwendo wa saa kumi na mbili jioni.

Mwanzoni mechi hiyo ilionekana kuishia sare tasa kwani timu zote mbili zilionekana kutoshana nguvu ila Tottenham wakabahatika kuponyoka na ushindi wa 0-1 katika dakika ya 96 kupitia mlinzi Davinson Sanchez.

Crystal Palace walipoteza nyumbani 2-3 dhidi ya West Ham United. Mabao mawili ya Manuel Lanzini na moja la Michail Antonio yalisaidia West Ham kupata ushindi. Odsonne Edouard na Michael Olise walifungua Palace.

Mechi nne zilichezwa Jumapili.

Everton waliendeleza fomu  yao mbaya kwa kupoteza nyumbani 2-3 dhidi ya Brighton.  Mabao mawili ya Alexis Mac Allister na moja la Dan Burn yaliangamiza vijana wa Rafa Benitez ambao walifungiwa mawili na Antony Gordon.

Brentford waliwika nyumbani dhidi ya Aston Villa na kuandikisha ushindi wa 2-1. Yoane Wissa na Mads Roerslev Rasmussen walifungia Brentford huku Danny Ings akifunga bao la pekee la Villa.

Leeds walipata ushindi wa 3-1 nyumbani dhidi ya Burnley kupitia mabao ya Jack Harrison, Stuart Dallas na Daniel James. Maxwel Cornet alifunga bao la Villa.

Mechi kubwa ya Jumapili iliyokuwa imesubiriwa sana kati ya Chelsea na Liverpool ugani Stamford Bridge iliishia sare ya 2-2.

The Blues walionekana kulemewa nguvu katika dakika za kwanza na kucharazwa kwa mabao mawili ila wakafufuka katika dakika tano za kufunga kipindi cha kwanza ambapo waliweza kusawazisha.

Sadio Mane na Mohammed Salah walifungia Liverpool huku mabao ya Chelsea yakifungwa na Mateo Kovacic na Christian Puliic.

Mechi mbili zilizopaswa kuchezwa wikendi iliyotamatika ziliahirishwa kufuatia visa vya COVID-19 miongoni mwa wachezaji wa timu husika.   Mechi zilizoahirishwa ni ile ya  Leicester vs Norwich pamoja na Southampton v Newcastle.

United watamenyana na Wolves mwendo wa saa mbili unusu usiku wa Jumatatu ugani Old Trafford.