Beki Thiago Silva aongeza mkataba wake Chelsea

Muhtasari

•Mbrazili huyo mwenye umri wa miaka 37 aliongeza mkataba wake na The Blues kwa mwaka mmoja mnamo Jumatatu

•Mkurugenzi wa Chelsea Marina  Granovskaia amemsifia mlinzii huyo kwa uzoefu na mchezo wake bora huku akisema atakuwa kiungo muhimu katika klabu hiyo msimu huu na msimu uja

Thiago Silva ameongeza mkataba wake Chelsea kwa mwaka mmoja
Thiago Silva ameongeza mkataba wake Chelsea kwa mwaka mmoja
Image: CHELSEA

Beki matata Thiago Silva sasa atasalia katika klabu ya Chelsea hadi msimu ujao wa 2022/23.

Mbrazili huyo mwenye umri wa miaka 37 aliongeza mkataba wake na The Blues kwa mwaka mmoja mnamo Jumatatu, Januari 3, 2022.

Silva ambaye alijiunga na klabu hiyo mwaka wa 2020 ameendelea kushangaza wengi na fomu yake nzuri licha ya umri wake mkubwa.

Beki huyo ambaye amewakilisha The Blues katika mechi 56 kufikia sasa alisema anafurahia sana kuweza kuongeza mkataba wake pale.

"Kucheza hapa na Chelsea ni furaha ya kweli. Sikuwahi kufikiria ningecheza kwa miaka mitatu hapa katika klabu hii kubwa kwa hivyo nina furaha sana kubaki kwa msimu mwingine" Thiago alisema.

Mkurugenzi wa Chelsea Marina  Granovskaia amemsifia mlinzii huyo kwa uzoefu na mchezo wake bora huku akisema atakuwa kiungo muhimu katika klabu hiyo msimu huu na msimu ujao.

"Uzoefu, uongozi na uchezaji wa Thiago Silva umekuwa na umesalia kuwa muhimu sana kwa kikosi hiki, kwa hivyo tunayo furaha kubwa kuongeza mkataba wake kwa mwaka mwingine. ‘Tunategemea ushawishi wake unaoendelea tunapotafuta mataji msimu huu na ujao, na zaidi ya sifa ambazo zimempelekea kuwa na mchango mkubwa kwetu ndani na nje ya uwanja" Alisema.

Kufuatia hayo Silva sasa ataondoka Chelsea baada ya msimu wa 2022/23 kukamilika.