Frank Lampard ateuliwa kama meneja wa Everton mwaka mmoja baada ya kutimuliwa na Chelsea

Muhtasari

•Lampard alitia saini mkataba wa miaka miwili unusu na klabu hiyo na utakamilika mnamo Juni 2024.

Everton yamteua Lampard kama kocha mpya
Everton yamteua Lampard kama kocha mpya
Image: EVERTON.COM

Klabu ya Everton imekamilisha uteuzi wa aliyekuwa kocha wa Chelsea, Frank Lampard kama meneja wake mpya.

Everton ilitangaza uteuzi wa kiungo huyo wa zamani wa Uingereza na The Blues kama meneja mpya siku ya Jumatatu kupitia tovuti rasmi ya klabu.

Lampard alitia saini mkataba wa miaka miwili unusu na klabu hiyo na utakamilika mnamo Juni 2024.

Mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 43 na ambaye amekaa bila nje ya taaluma ya ukufunzi kwa takriban mwaka moja baada ya kutimuliwa na Chelsea amesema ako tayari kuchukua jukumu alilokabidhiwa na Toffees.

"Ni heshima kubwa kwangu kuwakilisha na kusimamia klabu yenye ukubwa na utamaduni wa Klabu ya Soka kama Everton. Nina njaa sana ya kuanza. Baada ya kuzungumza na mmiliki, Mwenyekiti na Bodi, nilihisi sana shauku na matarajio yao" Lampard alisema.

Haya yanajiri takriban wiki mbili tu baada ya Everton kumtimua aliyekuwa kocha Rafael Benitez kufuatia msururu wa matokeo hafifu.

Lampard pia alipigwa kalamu na klabu yake ya zamani Chelsea mnamo Januari mwaka jana baada ya kushindwa kuafikia matarajio ya wamiliki klabu na mashabiki.