Gor yamteua Andreas Spier kama mkufunzi mpya

Muhtasari

• Timu ya Gor Mahia yamteua Mjerumani Andreas Spier kama mkufunzi mpya, siku chache baada ya kusitisha mkataba wa kocha muingereza Mark Harrison.

• Awali, kocha Andreas Spier alifanya kazi nchini Kenya katika shirikisho la soka FKF, alipohudumu kama mkurugenzi wa kiufundi, kitengo ambacho alifanikisha shughuli nyingi na imu ya taifa ya vijana wasiozidi umri wa miaka 18.

Kocha Andreas Spier akizinduliwa Gor Mahia
Image: Gor Mahia (Facebook)

Timu ya Gor Mahia imemteua Mjerumani Andreas Spier kama mkufunzi mpya, siku chache baada ya kusitisha mkataba wa kocha muingereza Mark Harrison.

Kupitia kwa ripoti zilizochapishwa katika tovuti ya timu hiyo Februari 1, Gor imempa Spier kandarasi kama mkufunzi mkuu huku akitarajiwa kusaidiwa na Michael Nam katika safu ya kiufundi ya timu hiyo.

Kocha Spier anajulikana katika ukanda wa Afrika mashariki kwa kuiongoza timu ya APR ya Rwanda hadi kutwaa ubingwa wa ligi kuu nchini humo kati ya mwaka wa 2013-2014.

Awali, kocha Andreas Spier alifanya kazi nchini Kenya katika shirikisho la soka FKF, alipohudumu kama mkurugenzi wa kiufundi, kitengo ambacho alifanikisha shughuli nyingi na timu ya taifa ya vijana wasiozidi umri wa miaka 18.

Mjerumani huyo ambaye ana leseni ya kuhudumu kama kocha mkuu kutoka kwa shirikisho la soka barani uropa, UEFA, pia amewahi kuwa mkurugenzi wa kiufundi wa shirikisho la soka nchini Rwanda, FERWAFA.

“Kufikia leo ambapo tumempa kandarasi na mikoba ya kuiongoza timu ya Gor Mahia, Spier amekuwa akihudumu kama mkurugenzi wa kiufundi huko Hangzhou kama mshauri wa kimataifa wa maendeleo ya soka nchini China, katika mkoa wa Zhejiang,” Gor ilieleza.

Kwa upande wa kocha msaidizi Nam, ambaye anatarajiwa kushirikiana na kocha mkuu Spier, Gor imemsifia pia kwa mapana.

“Nam ana uzoefu mkubwa katika ligi za nyumbani huku akiwa amehudumu katika timu za Homegrown FC, Agro-Chemicals na Talanta FC. Nam pia aliongoza timu ya Vipers FC hadi kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi kuu nchini Uganda kabla ya kugura na kuelekea nchini Sudan Kusini alikoisaidia timu ya Altabara kutwaa ubingwa wa mwaka 2021,” Gor walimsifia.

Wawili hao wanatarajiwa kuleta uzoefu wao katika timu ya Gor na kufufua matumaini yao ya kuwania ubingwa wa ligi kuu nchini baada ya msururu wa matokeo mabaya yaliyosababisdha kocha wa awali Mark Harrison Pamoja na benchi lake la kiufundi kufutwa kazi.