Mabadiliko katika Gor huku Shakava akivuliwa unahodha

Muhtasari

• Baada ya uzinduzi wa kocha mpya Mjerumani Andreas Spiers pamoja na msaidizi wake Michael Nam, timu ya Gor Mahia imetangaza msururu wa mabadiliko timuni humo

• Gor Mahia wametangaza mabadiliko katika uongozi wa michezaji katika safu mbali mbali.

Kiungo Philemon Otieno na mlinda lango Boniface Oluoch
Image: Gor Mahia (Facebook)

Baada ya uzinduzi wa kocha mpya Mjerumani Andreas Spiers pamoja na msaidizi wake Michael Nam, timu ya Gor Mahia imetangaza msururu wa mabadiliko timuni humo.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ya timu hiyo, Gor Mahia wametangaza mabadiliko katika uongozi wa wachezaji katika safu mbali mbali.

Miongoni mwa mabadiliko ni kwamba nahodha Harun Shakava amenyang’anywa kiraba cha unahodha na kukabidhiwa kiungo Philemon Otieno huku naibu wake akiwa ni Samuel Onyango.

Mabadiliko mengine ni kwamba Gor imemteua mlinda lango Boniface Oluoch kuwa mkufunzi wa walinda lango, na Oluoch anakabidhiwa jukumu hilo kama mkufunzi wa mpito baada ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa makipa wa timu hiyo, Jerem Onyango.

Klabu ya Gor pia imesema kuwa hata ingawa Oluoch amepokezwa ukufunzi wa makipa, bado kocha mkuu wa timu ana uhuru wa kumteua na kumchezesha katika kikosi cha Gor.

Mabadiliko haya yanajiri saa chache tu baada ya timu hiyo kutangaza kocha mpya.