Beki wa Harambee Stars Joash Onyango afunguka kuhusu familia yake

Muhtasari

•Joash alisema anaipenda na kuithamini familia yake sana na anaamini kuwa mkewe anaendelea kuwatunza mabinti wao vizuri.

•Beki huyo ambaye alihitimu miaka 31 mnamo Jumatatu pia alifichua kuwa yeye sio shabiki mkubwa wa wanamuziki wa hapa nchini.

Beki wa Harambee Stars na Simba Joash Onyango, 31
Beki wa Harambee Stars na Simba Joash Onyango, 31
Image: HISANI

Beki matata wa timu ya taifa ya Harambee Stars Joash Onyango amefunguka kuhusu mambo mbalimbali ya maisha yake.

Alipokuwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Joash aliweka wazi kwamba kando na kucheza kabumbu yeye pia ni mwanafamilia.

Joash ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Simba nchini Tanzania alifichua kuwa ako katika ndoa  na tayari ako na watoto wawili.

"Mimi niko katika ndoa, nimebarikiwa na mabinti wawili. Wa kwanza ana miaka mitano na wa pili ana mwaka mmoja" Joash alisema.

Joash alisema anaipenda na kuithamini familia yake sana na anaamini kuwa mkewe anaendelea kuwatunza mabinti wao vizuri.

Beki huyo ambaye alihitimu miaka 31 mnamo Jumatatu pia alifichua kuwa yeye sio shabiki mkubwa wa wanamuziki wa hapa nchini. Hata hivyo alisema anamshabikia Otile Brown na msanii mwenzake kutoka Bongo Ali Kiba.

"Hata kama huwa siwashabiki wanamuziki wa huko sana, nampenda Otile Brown. Mimi ni shabiki wa Alikiba, yeye ni mtu mtulivu, anatia bidii. Jinsi huwa anajiendeleza na muziki wake, huwa hana haraka, nampendea hayo" Alisema.

Onyango aliweka wazi kwamba yeye ni shabiki sugu wa nyimbo aina ya reggea.