"Kuondoka bila kwaheri kunaumiza" Aubameyang aaga mashabiki wa Arsenal kwa ujumbe wa kihisia

Muhtasari

•Mshambulizi huyo amewashukuru mashabiki wa Arsenal kwa ushirikiano mzuri na uungaji mkono wao.

•Amesema licha ya changamoto zilizomkuba katika siku zake za mwisho na klabu hiyo ataendelea kuihifadhi moyoni na kuipa heshima kubwa.

Pierre-Emerick Aubameyang
Pierre-Emerick Aubameyang
Image: GETTY IMAGES

Mshambulizi Pierre-Emerick Aubameyang amezungumza kwa mara ya kwanza baada ya mkataba wake na Arsenal kukatizwa kwa makubaliano ya pande zote mbili.

Katika ujumbe alioandikia mashabiki wa klabu hiyo ya London, Aubameyang amekiri kwamba inauma sana kuondoka bila kuwaaga vizuri.

Raia huyo wa Gabon ambaye alijiunga na Barcelona siku ya Jumatatu amewashukuru mashabiki wa Arsenal kwa ushirikiano mzuri na uungaji mkono wao.

"Kwa mashabiki wa Arsenal, asanteni kwa kuifanya London iwe nyumbani kwangu na familia yangu kwa miaka minne iliyopita. Tulipitia heka heka pamoja na uungaji mkono wenu ulimaanisha kila kitu kwangu. Kuwa na nafasi ya kushinda mataji na heshima ya kuwa nahodha wa klabu hii ni jambo ambalo nitaliweka moyoni mwangu milele" Auba aliandika.

Mshambulizi huyo matata mwenye umri wa miaka 32 amesisitiza kuwa siku zote amekuwa akimakinika na kujitolea kusaidia klabu ya Arsenal kufikia mafanikio zaidi.

Amesema licha ya changamoto zilizomkuba katika siku zake za mwisho na klabu hiyo ataendelea kuihifadhi moyoni na kuipa heshima kubwa.

"Siku zote nimekuwa nikimakinika 100% na kujitolea kufanya kila niwezalo kwa klabu hii ndiyo maana kuondoka bila kuaga kweli inaumiza - lakini ndio soka. Nina huzuni sikupata nafasi ya kusaidia wachezaji wenzangu katika wiki chache zilizopita, lakini sina kingine ila heshima kwa klabu hii na ninawatakia kila la heri vijana wangu na mashabiki wote. Kheri na miaka mingi yenye mafanikio katika siku zijazo! Upendo, Auba" Amesema.

Aubameyang alijiunga na Barcelona katika siku ya mwisho ya dirisha la uhamisho la Januari kwa uhamisho huru baada ya mkataba wake na Arsenal kutamatishwa.