Senegal yaingia fainali baada ya kuwalemea Burkina Faso

Muhtasari

• Timu ya taifa ya Senegal imejikatia tikiti katika fainali za AFCON 2022 baada ya kuwachabanga Burkina Faso mabao matatu kwa moja.

• Hii imekuwa ni mara yao ya pili mtawalia kutinga katika fainali hizo baada ya kuibuka washinde katika kipute cha AFCON cha mwaka wa 2019 dhidi ya mbweha wa jangwani, Algeria.

Total Energies African Cup of Nations
Image: Facebook

Timu ya taifa ya Senegal imejikatia tikiti katika fainali za AFCON 2022 baada ya kuwachabanga Burkina Faso mabao matatu kwa moja.

Hii imekuwa ni mara yao ya pili mtawalia kutinga katika fainali hizo baada ya kuibuka washinde katika kipute cha AFCON cha mwaka wa 2019 dhidi ya mbweha wa jangwani, Algeria.

Senegal walifungua ukurasa wa magoli baada ya mpira wa kona kupigwa na kumkuta mkabaji wa kati wa timu ya Ufaransa PSG, Abdou Diallo aliyejinafasi vizuri katika kijisanduku na kuelekeza mpira wavuni baada ya dakika sitini na tisa za mchezo.

Bao la pili la Senegal lilifungwa na kiungo Idrissa Gueye baada ya mshambulizi matata Sadio Mane kummegea pasi nyeresi kunako dakika ya sabini na sita kabla ya Mane tena kufunga la tatu na kuwahakikishia Senegal nafasi katika fainali ya kipute hicho.

Timu ya Burkina Faso walipata bao la kifuta machozi kunako dakika ya 82 kutoka kwa mchezaji Toure.

Senegal sasa wanasubiria mshindi kati ya timu ya taifa ya Misri na wenyeji wa kipute cha AFCON, Cameroon. Fainali za kombe hilo zitachezwa Februari 6 katika uga wa Olembe jijini Yaounde.