Shakava ajiunga na Polisi baada ya kuvuliwa unahodha Gor

Muhtasari

• Aliyekuwa nahodha wa timu ya Gor Mahia Harun Shakava amegura timu hiyo na kujiunga na malimbukeni Police FC

• Shakava alitambulishwa na Police FC na kukabidhiwa jezi nambari 18 baada ya kusaini kandarasi ya mwaka mmoja akiitumikia timu ya polisi.

Police FC
Image: Facebook

Aliyekuwa nahodha wa timu ya Gor Mahia Harun Shakava amegura timu hiyo na kujiunga na malimbukeni Police FC, siku chache baada ya timu ya Gor kutangaza mabadiliko ambapo Shakava alivuliwa cheo cha unahodha na kukabidhiwa kiungo Philemon Otieno.

Shakava alitambulishwa na Police FC na kukabidhiwa jezi nambari 18 baada ya kusaini kandarasi ya mwaka mmoja akiitumikia timu ya polisi.

Mkataba huo pia ulikuwa na kifungu cha Shakava kuongezewa mkataba wa kustaafu na huduma ya polisi kwa taifa.

Timu ya Police FC ikionesha kufurahi kwao baada ya kumnasa kiungo huyo, wameandika,

“Kuna polisi mpya mjini, Harun Shakava,”

Timu ya polisi ambayo ilibandishwa daraja ya kushiriki katika ligi kuu nchini Kenya msimu huu wamefanya usajili wa wachezaji kadha wenye majina tajika kama vile Eric Juma kutoka Kariobangi Sharks, aliyekuwa kiungo wa Yanga kutoka Tanzania, Francis Kahata, David Owino miongoni mwa majina mengi tajika.