Kocha Aliou Cisse asifiwa kwa kuiongoza Senegal kutwaa taji la kwanza la Afcon

Muhtasari

•Cisse amesifiwa kama kocha Mwafrika aliyeruka vikwazo vyote na kusaidia timu yake kunyakua mojawapo ya mataji makubwa zaidi duniani.

•Miongo miwili iliyopita, Cisse alikuwa nahodha wa kikosi cha Simba wa Teranga ambacho kilipoteza katika fainali ya Afcon dhidi ya Cameroon.

Kocha wa Senegal Aliou Cisse
Kocha wa Senegal Aliou Cisse
Image: HISANI

Kocha wa Senegal Aliou Cisse amepongezwa sana kufuatia ushindi wao wa taji la Afcon 2021 siku ya Jumapili.

Mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 45 aliongoza taifa lake kunyakua taji la kwanza la Afcon kwa kuibwaga Misri katika fainali iliyochezwa ugani Yaoundé’s Olembe , Cameroon.

Cisse amesifiwa kama kocha Mwafrika aliyeruka vikwazo vyote na kusaidia timu yake kunyakua mojawapo ya mataji makubwa zaidi duniani.

Miongo miwili iliyopita, Cisse alikuwa nahodha wa kikosi cha Simba wa Teranga ambacho kilipoteza katika fainali ya Afcon dhidi ya Cameroon.

Mchekeshaji mashuhuri Daniel Ndambuki almaarufu kama Churchill amemtambua Cisse kama gwiji kwa kusaidia taifa lake kunyakua taji la Afcon kama kocha baada ya kulikosa alipokuwa mchezaji.

"Gwiji huyu Aliou Cissé amenyanyua taji la Kombe la Afrika kama kocha baada ya kukosa kama mchezaji" Churchill alisema kupitia mtandao wa Twitter.

Mafanikio ya Cisse yameibua shinikizo kwa mataifa na klabu za Afrika kuwa na imani zaidi na makocha wa hapa barani.

Ushindi wa Senegal pia umetumiwa kama funzo la ukakamavu kwani taifa hilo limesubiri miaka mingi kunyakua taji la kwanza la Afcon. Hapo awali taifa hilo la Afrika Magharibi limecheza katika fainali mbili na kupoteza.

Senegal ilibwaga Egypt kupitia mikwaju ya penalti baada ya mchuano wa fainali kuishia sare tasa katika dakika za kawaida.