Kocha wa Chelsea Thomas Tuchel asema 'si wakati wa kumkejeli' Lukaku

Muhtasari

•"Yuko kwenye uangalizi na tutamlinda. Romelu daima atakuwa sehemu ya suluhisho," Tuchel alisema

Image: GETTY IMAGES

Mkufunzi wa Chelsea Thomas Tuchel amesema "hakuna wakati wa kumcheka" Romelu Lukaku baada ya mshambuliaji huyo aliyenunuliwa kwa kima cha takriban pauni milioni 97.5 kukabiliwa na changamoto uwanjani siku za hivi karibuni.

Lukaku alifanikiwa kugusa mpira mara saba tu katika mechi ya Jumamosi ambapo Chelsea ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Crystal Palace, kiwango ambacho ni cha chini kwa mchezaji yeyote kuwahi kugusa mpira katika dakika 90 za mechi ya Ligi ya Premia tangu mwaka 2003, wakati data hiyo iliporekodiwa mara ya kwanza.

"Yuko kwenye uangalizi na tutamlinda. Romelu daima atakuwa sehemu ya suluhisho," Tuchel alisema.

"Wakati mwingine inakuwa hivi kwa washambuliaji ikiwa wanajitahidi kidogo kujiamini na kutafuta nafasi ya kujihusisha na safu nzuri ya ulinzi.

"Bila shaka sio kile tunachotaka au anachotaka Lukaku lakini huu sio wakati wa kumcheka na kufanya masihara kumhusu."

Mshambuliaji huyo wa Ubelgiji wa miaka 28, amefanikiwa kufunga mabao matano pekee ya Ligi ya Primia katika mechi 17 tangu ajiunge tena na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Chelsea msimu huu, na kufunga mabao mengine matano katika mashindano mengine.