Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich awekewa vikwazo na Uingereza

Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich
Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich
Image: HISANI

Mmiliki wa klabu ya Chelsea, Roman Abramovich amewekewa vikwazo na serikali ya Uingereza kama sehemu ya majibu yake kwa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Yeye ni mmoja wa wafanyabiashara saba matajiri kuwekewa vikwazo vipya, ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kwa mali yao na marufuku ya kusafiri.

Orodha hiyo pia inajumuisha mabilionea Igor Sechin na Oleg Deripaska, wote wanaoonekana kuwa washirika wa Vladimir Putin.

Waziri Mkuu Boris Johnson alisema "hakuwezi kuwa na maeneo salama" kwa wale ambao wameunga mkono uvamizi huo.

"Vikwazo vya leo ni hatua ya hivi punde katika uungwaji mkono usioyumbayumba wa Uingereza kwa watu wa Ukraine. Tutakuwa watu wasio na huruma katika kuwasaka wale wanaowezesha mauaji ya raia, uharibifu wa hospitali na uvamizi haramu wa washirika huru," Bw Johnson alisema.

Serikali ilikuwa imekabiliwa na shinikizo la kumuwekea vikwazo Bw Abramovich, ambaye alisema alikuwa amefanya "uamuzi mgumu" wa kuiuza Chelsea FC mapema mwezi huu.

Abramovich, 55, anadaiwa kuwa na uhusiano wa karibu na Rais wa Urusi Vladimir Putin, jambo ambalo amelikanusha.

Serikali inasema Bw Abramovich, ambaye anakadiriwa kuwa na mali ya thamani ya £9.4bn, ni "mmoja wa matajiri wachache kutoka miaka ya 1990 kudumisha ushawishi chini ya Putin".