Chelsea yavunja kimya baada ya mmiliki wa klabu Roman Abramovich kuwekewa vikwazo na Uingereza

Muhtasari

•The Blues iliwahakikishia mashabiki kuwa serikali ya Uingereza imetoa leseni maalum itakayowaruhusu kuendeleza shughuli kadhaa ikiwemo kucheza.

•Vikwazo dhidi ya Abramovich vinamzuia kuuza klabu hiyo kwa sasa kama alivyokusudia kufanya hapo awali

Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich
Mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich
Image: HISANI

Klabu ya Chelsea imefahamisha mashabiki kuwa inafahamu kuhusu athari za masaibu yaliyokumba mmiliki wake Roman Abramovich.

Kupitia taarifa iliyotolewa Alhamisi, Chelsea ilikubali kwamba vikwazo dhidi ya mmiliki wake vitakuwa na athari mbaya kwa klabu. Hata hivyo, The Blues iliwahakikishia mashabiki kuwa serikali ya Uingereza imetoa leseni maalum itakayowaruhusu kuendeleza shughuli kadhaa ikiwemo kucheza.

"Chelsea imeshauriwa kuwa mmiliki wake Roman Abramovich amewekewa vikwazo na serikali ya Uingereza. Kwa mujibu wa umiliki wake wa asilimia 100 wa Chelsea FC  na mashirika tanzu, Chelsea FC kwa kawaida itaathirika na vikwazo dhidi ya  Bw Abramovich. Hata hivyo, Serikali ya Uingereza imetoa leseni maalum inayoruhusu Chelsea FC kuendelea na shughuli fulani," Taarifa ya Chelsea ilisoma.

Chelsea ilitangaza kuwa itashiriki mazungumzo zaidi na serikali ya Uingereza kuhusiana na faida za  leseni hiyo maalum. Hali kadhalika klabu hiyo itashirikisha serikali kwenye mazungumzo ya athari za vikwazo vya Abramovich.

Vikwazo dhidi ya Abramovich vinamzuia kuuza klabu hiyo kwa sasa kama alivyokusudia kufanya hapo awali.

Chelsea haiwezi tena kuuza tikiti za mechi baada ya hatua hii.  Wamiliki wa tikiti za msimu pekee ndio wanaweza kuhudhuria michezo kwa siku zijazo.

Hii pia inamaanisha hakutakuwa na mashabiki wa ugenini watakaoweza kuhudhuria mechi ugani Stamford Bridge kwa kipindi ambacho leseni inashikiliwa.

Hata hivyo Chelsea inaruhusiwa kuwalipa wachezaji, wakufunzi na wafanyikazi wake wengine licha ya vikwazo hivyo.