Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich awekewa sumu katika mazungumzo ya amani

Muhtasari

•Inaripotiwa huenda sumu inayodaiwa kuwewekewa bilionea huyo inahusishwa na watu wenye msimamo mkali nchini Urusi ambao walitaka kuhujumu mazungumzo hayo ya amani.

Roman Abramovich
Roman Abramovich
Image: BBC

Bilionea wa Urusi Roman Abramovich alikutwa na dalili zinazohusishwa na kuwekewa sumu katika mazungumzo ya amani katika mpaka wa Ukraine na Belarus mapema mwezi huu, vyanzo vya karibu naye vimesema.

Mmiliki huyo wa Chelsea FC - ambaye kwa sasa amesalimika - aliripotiwa kupata madhara kwenye macho na ngozi.

Wapatanishi wengine wawili wa amani katika mazungumzo ya Ukraine na Urusi kutoka Ukraine wanasemekana pia wameathirika.

Moja ya ripoti ilisema kuwa huenda sumu hiyo inayodaiwa kuwewekewa bilionea huyo inahusishwa na watu wenye msimamo mkali nchini Urusi ambao walitaka kuhujumu mazungumzo hayo ya amani.

Muda mfupi baada ya madai hayo kuibuka, afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutajwa jina lake alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa taarifa za kiintelijensia zinaashiria kuwa dalili za watu hao zilitokana na sababu za "mazingira", na sio sumu.

Na baadaye afisa katika ofisi ya rais wa Ukraine, Ihor Zhovkva, ameiambia BBC kuwa hajazungumza bado na Bw Abramovich, lakini wajumbe wa ujumbe wa Ukraine wako "salama" na mmoja alisema kuwa taarifa hizo za sumu ni "uongo".

Hata hivyo, mwandishi wa masuala ya usalama wa BBC Frank Gardner anasema kuwa si jambo la kushangaza kwamba Marekani kutaka kuondoa madai kwamba yoyote - hasa Urusi - ilikuwa ilitumia silaha ya kemikali nchini Ukraine, kwani hilo linaweza kuwasukuma katika hatua za kulipiza kisasi kitu ambacho wanasita kukikubali.

'Maumivu katika macho'

Hali ya Bw Abramovich na wapatanishi wa Ukraine, ambao ni pamoja na mbunge wa Ukraine Rustem Umerov, imeimarika tangu tukio hilo la Machi 3, jarida la Wall Street lilinukuu vyanzo vikisema.

Chanzo cha karibu na Bw Abramovich kimeiambia BBC kuwa sasa amepona na anaendelea na mazungumzo ya kujaribu kumaliza vita nchini Ukraine.

Tukio hilo linaangazia jukumu pia la Bw Abramovich kama mmoja wa wapatanishi katika mazungumzo a Amani kati ya Ukraine na Urusi.

"Hali halisi ya msimamo wake haijulikani, lakini msemaji wa tajiri huyo hapo awali alisema ushawishi wake ulikuwa "mdogo".

Bilionea huyo wa Urusi mara kadhaa alisafiri kati ya Moscow na Kyiv kwa ajili ya mazungumzo mwanzoni mwa mwezi huu. Aliripotiwa kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wakati wa ziara hizo, lakini kiongozi huyo wa Ukraine hakuathirika na msemaji wake hakuwa na taarifa kuhusu tukio hilo.

Kundi la uandishi wa habari za uchunguzi Bellingcat, wakati huo huo, lilisema Bw Abramovich na wapatanishi wengine walipatikana na dalili "zinazoambatana na sumu na silaha za kemikali".

Dalili hizo ni pamoja na "kuvimba kwa macho na ngozi na maumivu ya makali machoni", Bellingcat iliripoti.

Bw Abramovich ameonekana hadharani, akipigwa picha katika uwanja wa ndege wa Tel Aviv nchini Israel tarehe 14 mwezi Machi.

Image: REUTERS

Bw Abramovich aliwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya na Uingereza mapema mwezi huu kutokana na madai ya uhusiano wake wa karibu na rais wa Urusi Vladimir Putin, madai ambayo anayakanusha.

Lakini Bwana Zelensky ameripotiwa kuiomba Marekani kuachana na vikwazo dhidi ya Bw Abramovich, akidai kuwa anaweza kubeba jukumu la mazungumzo ya makubaliano ya amani na Moscow.

Kremlin imesema Bw Abramovich alianza kutekeleza jukumu hilo la mazungumzo ya amani hapo awali lakini mchakato huo kwa sasa uko mikononi mwa timu za mazungumzo za nchi hizo mbili.

Pande hizo zinatarajiwa kukutana leo Jumanne, ikwa ni kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya wiki mbili.

Nini Kilitokea hasa kwenye mazungumzo hayo?

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari za uchunguzi Frank Gardner, Mchana wa Machi 3, Roman Abramovich alijiunga na wapatanishi wengine wa amani wa Urusi na Ukraine katika mazungumzo kwenye mpaka wa Ukraine na Belarus. Katika uchambuzi wake anasema kilichotokea baadaye ni cha kushangaza.

Baadaye usiku huo, wajumbe watatu - ikiwa ni pamoja na Bw Abramovich - kwa mujibu wa tovuti ya uchunguzi ya Bellingcat, walipata dalili za sumu.

Walipatwa na matatizo ya ngozi iliyoonekana kama kubabuka, macho kuvimba na maumivu makali - dalili ambazo zilidumu usiku wote.

Kwa mujibu wa Bellingcat, hakuna hata mmoja kati yao aliyekula kitu kingine chochote zaidi chokoleti na maji.

Gardner anaasema wataalamu wa silaha za kemikali wamechunguza suala hili na kuhitimisha kuwa wanaamini kulikuwa na matumizi ya makusudi ya kemikali.

Lakini haijulikani ni nani aliyefanya hivyo. Hakuna aliyejitokeza kusema anawajibika na hilo.

Yapo madai mengine kwamba kilichotokea ni kwamba mtu alitaka kutoa onyo kwa wale wanaoshiriki katika mazungumzo ya amani. Ilikuwa sumu ya kiwango cha kawaida sio cha hatari, ilikuwa onyo.

Gardner anasema maoni yaliyotolewa na afisa wa Marekani ambaye hakutajwa jina lake kwamba sababu za mazingira ndizo sababu ya dalili walizopata kina Abramovich ni za kawaida.

Hakuna mtu mwingine aliyeathiriwa. Je mazingira yameathiri watu hao tu pekee kati ya makumi ya watu? Mtaalamu wa silaha za kemikali, Hamish De Bretton-Gordon, ameiambia BBC kuwa haiwezekani kwamba sababu za kimazingira zina uhusiano wowote na hilo.