Chelsea yapata mmiliki wapya baada ya kuwekwa sokoni

Muhtasari

•Baada ya kukamilisha malipo, wamiliki wapya watahitajika kuwekeza pauni bilioni 1.75 kwa manufaa ya klabu hiyo.

•Uuzaji wa klabu hiyo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mei chini ya idhini zote muhimu za udhibiti. 

Todd Boehly ataongoza kundi litakalomilliki Chelsea
Todd Boehly ataongoza kundi litakalomilliki Chelsea
Image: BBC

Chelsea imefanya makubaliano ya kuuzwa  kwa klabu hiyo kwa wamiliki wapya baada ya Roman Abramovich kuiweka sokoni.

Taarifa iliyochapishwa na klabu hiyo imesema kundi linaloongozwa na mabwenyenye Todd Boehly, Clearlake Capital na Mark Walter  litachukua usakani baada ya kukamilisha malipo ya pauni bilioni 2.5.

Aidhaa, baada ya kukamilisha malipo wamiliki hao wapya watahitajika kuwekeza pauni bilioni 1.75 kwa manufaa ya klabu hiyo.

"Hii inajumuisha uwekezaji katika Stamford Bridge, akademi, timu ya Wanawake na Kingsmeadow na kuendelea na ufadhili wa Chelsea Foundation," Taarifa ya Chelsea ilisoma.

Uuzaji wa klabu hiyo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mei chini ya idhini zote muhimu za udhibiti. 

Chelsea iliwekwa sokoni kabla ya mmiliki wake Roman Abramovich kuwekewa vikwazo kufuatia madai kuwa ana uhusiano na rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye anaendelea kukosolewa kwa kuvamia Ukraine.

Todd Boehly ambaye ndiye anayeongoza kundi linalokusudia kununu Chelsea anaripotiwa kuwa na utajiri wa dola bilioni 4.5 kulingana na Forbes. Yeye ni mmiliki mwenza wa timu ya besiboli ya LA Dodgers.

Uhamisho wa umiliki utahitaji idhini kutoka kwa mamlaka ya soka ya Uingereza na serikali ya Uingereza.