Kenya na Zimbabwe zazuiliwa kushiriki AFCON 2023

Muhtasari

•Mataifa yote mawili hayatashiriki mechi za kufuzu michuano hiyo mwezi ujao kwa sababu ya marufuku yao ya kutoshiriki soka la kimataifa.

Image: GETTY IMAGES

Zimbabwe na Kenya hazitashiriki Kombe la Mataifa ya Afrika 2023, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limetangaza.

Mataifa yote mawili hayatashiriki mechi za kufuzu michuano hiyo mwezi ujao kwa sababu ya marufuku yao ya kutoshiriki soka la kimataifa, iliyotolewa na Fifa kwa sababu ya serikali kuingilia shughuli za uendeshaji wa soka katika nchi hizo.

"CAF iliziweka [Kenya na Zimbabwe] katika droo rasmi mapema Aprili 2022 kwa sharti kwamba adhabu hiyo ( ya FIFA)iondolewe wiki mbili kabla ya mechi yao ya kwanza," ilisema taarifa ya Caf.

FIFA haijaziondolea marufuku nchi hizo.

Harambee Stars, ambayo mechi yao ya hivi majuzi zaidi ya Kombe la Mataifa ya Afrika ilikuwa mwaka wa 2019, ilikuwa icheze na Cameroon Juni 4 huku Zimbabwe, ambao wamekuwepo kwenye fainali tatu zilizopita, wakipangiwa kuwa mwenyeji wa Liberia siku tano baadaye.

Ina maana kuwa Kundi C ambalo Kenya ilikuwa imepangwa, sasa itaziacha Cameroon, Namibia na Burundi huku Kundi K la Zimbabwe likiwa limebaki na mataifa ya Morocco, Afrika Kusini na Liberia pekee. Timu mbili za juu zitasonga mbele.

Marufuku hiyo iliyowekwa na Fifa mwezi Februari ilikuja baada ya serikali za nchi zote mbili kuingilia kati kufuta mashirikisho yao.

Kenya ilishiriki mmara sita michuano ya AFCON wakati Zimbabwe ameshiriki fainali hizo mara tano.