'Serengeti Girls' wa Tanzania wafuzu kwa Kombe la Dunia

Muhtasari

•Timu hiyo ilifuzu baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 5-1 dhidi ya Cameroon.

Image: SERENGETI GIRLS

Timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 17 ya Tanzania ‘Serengeti Girls’ imefuzu kushiriki michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Oktoba mwaka huu nchini India.

Timu hiyo imefuzu baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 5-1 dhidi ya Cameroon. Serengeti ilipata ushindi wa bao 1-0 leo, bao lililowekwa kimiani na Neema Paul.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Cameroon, timu hiyo ilishinda kwa mabao 4-1.

Tanzania sasa imeungana na Morocco na Nigeria kuiwakilisha Afrika na kukamilisha idadi ya timu 16 zitakazoshiriki fainali hizo za Dunia kati ya Oktoba 11-30 mwaka huu katika miji mitatu nchini India zikiwa fainali za saba tangu michuano ilipoasisiwa mwaka 2008.

Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufuzu fainali hizo kwa timu za soka. Hadi kufuzu, Serengeti ilizing’oa Botswana, Burundi na kumalizia kwa kuitoa Cameroon.

Hata hivyo, kinara wa mabao wa hatua ya kufuzu ni Mtanzania, Clara Luvanga ambaye amefunga jumla ya mabao 10.