Lois Openda: Mfahamu mshambuliaji matata wa Ubelgiji anayedaiwa kuwa Mkenya

Muhtasari

•Mshambuliaji huyo chipukizi ameweza kubobea kiasi cha kufikia hatua ya kuitwa kwenye timu ya taifa ya Ubelgiji.

•Baadhi ya wanamitandao waliibua madai kuwa mshambuliaji huyo ni raia wa Kenya aliyeenda kutafuta riziki  Ulaya.

Lois Openda baada ya kufungia Ubelgiji katika mechi dhidi ya Poland
Lois Openda baada ya kufungia Ubelgiji katika mechi dhidi ya Poland
Image: HISANI

Lois Openda ni mshambuliaji matata mwenye umri wa miaka 22 ambaye anaichezea klabu ya Vitesse nchini Uholanzi.

Openda alizaliwa Februari 16, 2000 jijini Liege, Ubelgiji na wazazi kutoka Congo na Morocco ambao walikuwa wamehamia katika nchi hiyo ya Ulaya.

Timu ya taifa ya Ubelgiji:

Mshambuliaji huyo chipukizi ameweza kubobea kiasi cha kufikia hatua ya kuitwa kwenye timu ya taifa ya Ubelgiji.

Openda aliichezea Ubelgiji kwa mara yake ya kwanza kwenye mechi dhidi ya Poland Jumatano usiku na hata kufunga bao lake la kwanza akiwa na timu hiyo dakika ya 93.

Miaka ya hapo awali mshambuliaji huyo aliwahi kuchezea Belgium U16, Belgium U17, Belgium U18, Belgium U19, Belgium U21 na kufunga zaidi ya mabao 20 kwa jumla.

Klabu

Openda alijiunga na Club Brugge mwaka wa 2015 na kucheza mechi kubwa ya kwanza na klabu hiyo takriban miaka miwili baadae.

Mnamo Julai 21, 2020 mshambulizi huyo alijiunga na Vitesse ya Uholanzi kwa mkopo. 

Katika kipind icha misimu miwili ambacho Openda ameichezea Vitesse ameweza kufunga takriban mabao 30 na kupeana assist saba.

Openda alianza safari yake ya kandanda katika klabu ya Patro Othee FC kabla ya kujiunga na RFC Liege, Standard Liege, Club Brugge na hatimaye Vitesse.

Kuvuma kwake

Openda aliwasisimua Wakenya baada ya kufungia Ubelgiji bao la mwisho katika mechi yao dhidi ya Poland ambapo walishinda 6-1.

Baadhi ya wanamitandao waliibua madai kuwa mshambuliaji huyo ni raia wa Kenya aliyeenda kutafuta riziki  Ulaya.

Wengine walidai kuwa Openda ni Mbelgiji aliyezaliwa na wazazi kutoka Kenya.

Tazama baadhi ya mabao kali ya mshambuliaji huyo