The Gunners wamsajili 'Viera mpya'

Muhtasari

•The Gunners ilitangaza usajili wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 Jumanne kupitia kurasa zake rasmi.

•Kiungo huyo ambaye amesifiwa sana anaripotiwa kuigharimu klabu hiyo ya Uingereza kiasi cha takriban milioni 40.

Fabio Viera , 22
Fabio Viera , 22
Image: ARSENAL

Klabu ya Arsenal imekamilisha usajili wa kiungo wa kati Fabio Viera kutoka Porto.

The Gunners ilitangaza usajili wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 Jumanne kupitia kurasa zake rasmi.

"Fabio atavaa jezi namba 21 na kuungana na wachezaji wenzake wapya hivi karibuni kwa mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya. Kila mtu katika Arsenal anamkaribisha Fabio kwenye klabu," Arsenal ilitangaza kupitia tovuti.

Kiungo huyo ambaye amesifiwa sana anaripotiwa kuigharimu klabu hiyo ya Uingereza kiasi cha takriban milioni 40.

Akizungumza baada ya kukamilisha uhamisho, Viera alipongeza mafanikio ya awali ya klabu hiyo na kubainisha kuwa anafurahia kucheza pale.

"Nimefurahia, bila shaka. Hii ni hatua muhimu katika kazi yangu. Arsenal ni klabu kubwa na ya kihistoria, kwa hivyo ninafurahia kuwa hapa," Viera alisema.

Baadhi ya mashabiki wamemlinganisha kiungo huyo wa kati na nahodha wa zamani wa klabu hiyo Patrick Viera hasa kwa kuwa wanacheza nafasi sawa.

Katika msimu wa 2021/22 Viera alichezea Porto mechi 27 huku akifunga mabao 6 na kusaidia katika mabao 14.

Kimataifa kiungo huyo amehusishwa katika timu ya Kitaifa ya Portugal Under 21.