Beki matata Lisandro Martinez kujiunga na Mashetani Wekundu

Martinez anaripotiwa kuigharimu United pauni milioni 55 (Ksh 7.7B)

Muhtasari

•Jumapili jioni Mashetani Wekundu walitangaza kuwa wamefikia makubaliano na Ajax kuhusu uhamisho wa Muargentina huyo.

•United ilitangaza kwamba Martinez atajiunga nao baada ya makubaliano ya masharti na kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

Image: TWITTER// LISANDRO MARTINEZ

Klabu ya Ligi Kuu Uingereza, Manchester United imekamilisha usajili wa beki wa kati Lisandro Martinez kutoka Ajax.

Jumapili jioni Mashetani Wekundu walitangaza kuwa wamefikia makubaliano na Ajax kuhusu uhamisho wa Muargentina huyo.

"Manchester United inafuraha kutangaza kuwa klabu imefikia makubaliano na Ajax kuhusu uhamisho wa beki wa kimataifa wa Argentina Lisandro Martinez," United ilitangaza kupitia tovuti yake rasmi.

Klabu hiyo ya Uingereza pia ilitangaza kwamba mchezaji huyo matata mwenye umri wa miaka 24 atajiunga nao baada ya makubaliano ya masharti na kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu.

Martinez anaripotiwa kuigharimu United  pauni milioni 55 (Ksh 7.7B) na atatia saini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo.

Beki huyo alisafiri Ijumaa kuenda Manchester pamoja na ajenti na United wanatarajiwa kukamilisha mpango huo siku zijazo. Atakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa chini ya meneja mpya Erik ten Hag baada ya Tyrell Malacia na Christian Eriksen.

Baada ya kujiunga rasmi na United Lisandro atapigania nafasi yake na mabeki wengine wa kati wakiwemo nahodha Harry Maguire, Eric Bailly, Phil Jones, Axel Tuanzebe, Raphael Varane na Victor Lindelof.

Martinez alijiunga na Ajax ya Uholanzi mwaka wa 2019 na kushirikishwa kwenye  jumla ya mechi 120 katika kipindi cha misimu mitatu ambayo imepita.

Kabla ya kujiunga na Ajax, beki huyo alichezea Newell's Old Boys, Defensa y Justicia na Defensa y Justicia za Argentina.