Kwanini timu za Premier League zinawekeza bara la Asia

Asia pekee inatarajiwa kuchangia $1.4bn kati ya msimu ujao na 2025.

Muhtasari

•Timu za Ligi Kuu ya Uingereza kwa mara nyingine tena zinazunguka ulimwengu katika ziara za kabla ya msimu wa joto.

•Msimu huu joto wapinzani wa Ligi ya Primia Manchester United waliamua kuzuru Thailand na Australia, ambapo pia walicheza na Liverpool na Crystal Palace.

Shabiki wa Liverpool akiwa ameinua jezi ya timu kwenye mchezo huko Singapore
Shabiki wa Liverpool akiwa ameinua jezi ya timu kwenye mchezo huko Singapore
Image: BBC

"Sina dini, sina Mungu. Klabu ya soka ya Liverpool ndiyo dini yangu - ni maisha kwangu."

Vijay alizaliwa Singapore - karibu kilomita 11,000 (maili 6,800) kutoka uwanja wa Anfield wa Liverpool - na amekuwa akingojea tangu 2011 kwa timu yake kutembelea jiji lake la nyumbani. Sio yeye pekee.

Mapema mwezi huu zaidi ya mashabiki 50,000 waliujaza Uwanja wa Taifa wa Singapore kwa ajili ya mechi ya kirafiki kati ya Liverpool na Crystal Palace.

Baada ya miaka mitatu ya marufuku ya usafiri kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Covid, timu za Ligi Kuu ya Uingereza kwa mara nyingine tena zinazunguka ulimwengu katika ziara za kabla ya msimu wa joto.

Umuhimu wa kifedha wa safari hizi ni ngumu kupindukia. Wakati Manchester United iliposajili hasara ya mapato ya kibiashara ya karibu $56m (£46.8m) mnamo 2021, klabu hiyo ilisema "ilitokana na" usumbufu wa Covid, ambao ulijumuisha kughairiwa kwa ziara ya timu ya kwanza ya maandalizi ya msimu mpya nchini India.

Ombi la kimataifa

Msimu huu joto wapinzani wa Ligi ya Primia Manchester United waliamua kuzuru Thailand na Australia, ambapo pia walicheza na Liverpool na Crystal Palace.

Wakati huohuo, Tottenham Hotspur ilisafiri Korea Kusini, ambako ni nchi ya nyumbani kwa mshambuliaji wao nyota Son Heung-min.

Kwa mtazamo wa michezo, safari hizi hazina maana. Safari ndefu za ndege katika maeneo kadhaa ya saa, halijoto ya juu na hali ya hewa yenye unyevunyevu si maandalizi bora kwa msimu mpya wa kurudi nyumbani Uingereza.

"Sio jambo ninalopenda kufanya," meneja wa Liverpool Jurgen Klopp, akijibu swali kutoka kwa BBC katika mkutano na waandishi wa habari.

"Kwanza kabisa mimi ni kocha na kama tunaweza kuzuru Austria wiki mbili na kufanya mazoezi mara mbili kwa siku nchini humo, itakuwa bora zaidi."

"Lakini tunajua jinsi mashabiki wetu walivyo wengi barani Asia na kuwa karibu nao ni jambo zuri sana."

Kiuhalisia , mjadala kama huu miongoni mwa wataalamu wa soka ulipata ufumbuzi muda mrefu uliopita.

Hoja ya kibiashara imeshinda kwa ukamilifu na watendaji msimu huu wa joto wana kila la kujivunia uamuzi huo kutokana na mwitikio mkubwa wa mashabiki wa soka katika maeneo hayo.

Takwimu mpya zilizoripotiwa mwaka huu zinaonyesha kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa, Ligi Kuu itapokea mapato zaidi kutoka kwa chaneli za kimataifa kuliko itakavyopokea kutoka kwa chaneli za ndani katika soko lake la nyumbani la Uingereza.

Asia pekee inatarajiwa kuchangia $1.4bn kati ya msimu ujao na 2025.

Huko Korea Kusini, mechi ya maonyesho ya Spurs dhidi ya nyota wa ndani iliuzwa ndani ya dakika 25.Pia likawa tukio la michezo lililotiririshwa zaidi katika historia ya nchi.

Wakati huohuo, mapromota mjini Bangkok walijisikia raha kuweka bei ya tikiti ya kuanzia kwa mechi ya kirafiki kati ya Manchester United na Liverpool kwa $136. Huko Singapore, tikiti za bei rahisi zinagharimu $107.

Tottenham Hotspur ilicheza nchini Korea Kusini, nchi ya nyumbani kwa mshambuliaji wao nyota Son Heung-min

Bei hizi ni za juu zaidi kuliko ile ambayo ingetarajiwa kulipwa na mashabiki nchini Uingereza kwa mechi ya ushindani, lakini hatimaye zinawakilisha mvuto mkubwa wa vilabu vikuu vya Ligi ya Premia.

Msemaji wa Liverpool aliiambia BBC: "Hatukuweka bei hizi za tikiti, tunapokea ada iliyowekwa, na hatupokei sehemu yoyote ya mapato ya tikiti."

Kiwango cha fedha kinachopokewa na timu hupokea kwa mechi hizi za kirafiki za mbali huwa vigumu kubaini na ni siri ambayo inapewa ulinzi wa karibu katika tasnia, lakini wachambuzi wanasema kuwa ada hizo haziwezi kuhalalisha safari pekee, haswa wakati gharama za usafiri na wafanyikazi zinazingatiwa.

"Timu hazipati pesa nyingi moja kwa moja kutokana na michezo ya kabla ya msimu, labda dola milioni chache kwa kila mechi katika kiwango cha juu kabisa," alisema Kevin McCullagh, mhariri wa kampuni ya Asia-Pacific ya uchapishaji wa biashara ya SportBusiness.

"Lakini kuna mchezo mkubwa zaidi. Hii ni kuhusu ujenzi wa chapa na ushiriki wa mashabiki katika soko ambalo litatoa mapato makubwa zaidi ya muda mrefu kutoka kwa mikataba ya haki za utangazaji na mikataba ya ufadhili na chapa na makampuni ya Asia. Hapo ndipo pesa halisi zinapatikana. "

Wakiwa Singapore, Liverpool walitia saini mkataba mpya wa udhamini wa jezi, unaoripotiwa kuwa na thamani ya zaidi ya $240m, na Standard Chartered, benki inayolenga Asia.

Mbali na kusaidia kuinua wasifu wa wafadhili kwenye jukwaa la kimataifa, vilabu vya soka vinaweza pia kuwapa hazina zilizotengenezwa tayari za data ya watumiaji.

Manchester United, kwa mfano, inakadiria kuwa hifadhidata yao ya usimamizi wa uhusiano wa wateja (CRM) ina rekodi za 50m.

Katika mitandao ya kijamii mwaka jana walikuwa na miunganisho ya milioni 176.

Hata hivyo, ni pesa za televisheni ambazo zimepandisha soka la Uingereza kileleni kifedha.

Kwa miaka mingi ligi zingine za michezo - zikiwemo ligi za kandanda za Ulaya - zimeitazama kwa kijicho Ligi Kuu, japo walikuwa wa kwanza kuja Asia na kuanzisha uhusiano wa kibiashara katika miaka ya 1990.

Ushindani wa Ligi Kuu, utamaduni tofauti wa mashabiki na ushirikiano na lugha ya Kiingereza vyote vimechangia kuwa ligi ya michezo inayotazamwa zaidi dunini, na kuvutia jumla ya watazamaji bilinii 3.2 duniani.