Mwanasoka amtuma nduguye kumwakilisha katika harusi yake huku akiwahi kusaini mkataba Malmo FC

"Kwanza, tutashinda ligi, halafu nitaenda fungate," Turay alisema

Muhtasari

• 'Tulifunga ndoa Julai 21 huko Sierra Leone. Lakini sikuwapo kwa sababu Malmo aliniomba nifike mapema.' - Buya Turay

Mwanasoka Mohamed Buya Turay akiwa na mkewe kabla ya kuondoka kwenda Uswidi
Mwanasoka Mohamed Buya Turay akiwa na mkewe kabla ya kuondoka kwenda Uswidi
Image: Twitter//Mohamed Buya Turay

Katika maisha ya binadamu, vipo vipengele vitatu muhimu ambavyo angalau kila mwanadamu lazima avipitie, navyo ni kuzaliwa, kuoa au kuolewa na hatimaye kufa.

Kila kipengele ni muhimu kwa nafasi yake, na haswa kuoa au kuolewa kwa sababu hay ani matukio yanayotokea kwa mtu wakati ashajitambua na kujielewa kufanya maamuzi huru.

Katika kuoa, harusi ni kitu kinachomhusu mtu moja kwa moja na kamwe hufai kukosa kwani wewe ndiwe mhusika mkuu.

Lakini nchini Sierra Leone, hili ni tofauti kwa familia ya mwanasoka mmoja kwa jina Mohammed Buya Turay ambaye siku yake ya harusi ilishabihiana na siku ambayo alitakikana kuwahi katika klabu ya Malmo chini Sweden ili kuandikisha mkataba wa kutumikia timu hiyo.

Cha kushangaza ni kwamba Buya Turay alichagua kuwahi kutia kandarasi katika klabu ya Malmo na badala yake akamtwika ndugu yake kusimama kama bwana arusi kwa niaba yake.

Turay aliliambia gazeti la Uswidi Aftonbladet: 'Tulifunga ndoa Julai 21 huko Sierra Leone. Lakini sikuwapo kwa sababu Malmo aliniomba nifike mapema.'

Turay ambaye alikuwa amepiga picha na mkewe wakiwa wamevalia mavazi ya harusi kabla ya kuondoka kuelekea Uswidi na kuzichapisha kwenye Twitter.

"Tulipiga picha hapo awali, kwa hivyo inaonekana kama nilikuwepo, lakini sikuwepo. Kaka yangu alipata kuniwakilisha kwenye harusi halisi,’' alisema kwenye Twitter.

Mwanasoka huyo aliandika kwenye Twitter kusherehekea ndoa hiyo ambayo aliwakilishwa na kaka yake, kwani kweli ndugu ni kufaana katika dhiki na Faraja.

“Nimeoa mchumba wangu, mke na rafiki yangu wa karibu leo!!! Ni binadamu wa ajabu sana!!! Na ni baraka iliyoje!!! Bibi SBT💞💍 Suad Baydoun. Siwezi kusubiri kufurahia maisha na wewe pamoja soboti,” Turay aliandika kweney Twitter.

Hajaunganishwa tena na mke wake tangu ndoa yao lakini aliahidi kuwa watafunga ndoa pamoja - hatimaye.

"Kwanza, tutashinda ligi, halafu nitaenda fungate," Turay alisema huku akitabasamu.