Rasmi! Makubaliano yaafikiwa kuhusu uhamisho wa Casemiro kujiunga na Mashetani Wekundu

Casemiro ameigharimu Manchester United Euro milioni 60 na nyongeza na Euro milioni 10.

Muhtasari

•Manchester United imefikia makubaliano na Real Madrid kuhusu uhamisho wa kiungo matata Carlos Henrique Casemiro.

•Real Madrid tayari imemuaga kiungo huyo na kusherehekea ushindi alioupata tangu ajiunge nao Januari 2013.

Image: INSTAGRAM// CASEMIRO

Klabu ya Manchester United imefikia makubaliano na Real Madrid kuhusu uhamisho wa kiungo matata Carlos Henrique Casemiro.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa jioni, United ilitangaza kuwa mchezaji huyo wa timu ya kitaifa ya Brazil mwenye umri wa miaka 30 atajiunga nao rasmi baada ya makubaliano ya masharti ya kibinafsi.

"Tunatazamia kumkaribisha Casemiro Old Trafford," Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya United ilisoma.

Casemiro anaripotiwa kuwagharimu Mashetani Wekundu Euro milioni 60 na nyongeza na Euro milioni 10.

Amekubali kutia saini mkataba wa miaka minne hadi 2027  na anatazamiwa kusafiri hadi Mancheter wikendi hii kwa ajili ya vipimo vya kidaktari.

Real Madrid tayari imemuaga kiungo huyo na kusherehekea ushindi alioupata tangu ajiunge nao Januari 2013.

"Real Madrid ingependa kutoa shukrani za dhati kwa Casemiro, ambaye ni sehemu ya historia ya klabu hii," Mabigwa hao wa Uhispania walisema katika taarifa.

Klabu hiyo pia ilitangaza kuwa hafla ya kumuaga rasmi Casemiro itafanyika Jumatatu kisha ahutubie waandishi wa habari.

"Real Madrid ndio nyumbani kwake na daima, na tunamtakia kila la heri yeye na familia yake katika sura hii mpya ya maisha yake."

Usajili huu umejiri huku Mashetani Wekundu wakitazamiwa kucheza na Liverpool Jumatatu. Klabu hiyo itatumai kuwa kiungo huyowa kati  mwenye kipawa ataweza kushiriki katika mechi hiyo kali itakayochezewa Old Trafford.