Erik ten Hag: 'Ninamuamini Maguire'

"Ninamuunga mkono kwa sababu ninamwamini," alisema Ten Hag.

Muhtasari

•Maguire amekuwa akidhihakiwa na baadhi ya mashabiki wake kwenye majukumu ya klabu na nchi msimu huu 

Harry Maguire
Image: BBC

Meneja wa Manchester United Erik ten Hag anasema bado anamuamini Harry Maguire licha ya beki huyo kukosolewa

Maguire amekuwa akidhihakiwa na baadhi ya mashabiki wake kwenye majukumu ya klabu na nchi msimu huu na alifanya makosa katika ufungaji wa mabao mawili ya Ujerumani katika sare ya 3-3 ya England siku ya Jumatatu.

"Ninamuunga mkono kwa sababu ninamwamini," alisema Ten Hag.

"Inamhusu. Nina hakika anaweza kufanya hivyo. Ataligeuza hili. Nina hakika sana kuhusu hilo."

Ten Hag amewapendelea Lisandro Martinez na Raphael Varane kama safu yake ya ulinzi ya kati, huku mchezaji Bruno Fernandes akivalia kitambaa cha unahodha mbele ya Maguire katika wiki za hivi karibuni.

Maguire amecheza mechi tatu pekee za Premier League msimu huu.

"Hata baada ya kutokuwa kwenye timu, alifanya mazoezi vizuri," alisema mkufunzi Ten Hag kuhusu mchezaji huyo mwenye wa umri wa miaka 29 .

"Lakini muhimu zaidi, ubora ulikuwepo. Unaona kazi yake, takribani mechi 50 akiwa na England. Amefanya vizuri sana kwa Leicester na Manchester United. Unachokiona ni kwamba ana uwezo wa juu."

Luke Shaw, mchezaji mwenza wa Manchester United na Uingereza, alisema mapema wiki hii kwamba Maguire amekosolewa "zaidi ya nilivyowahi kuona hapo awali kwenye soka".