(+video) Jinsi Ronaldo alionesha hisia usoni United ikizamishwa na City

Katika mechi hiyo ambayo United ilipigwa 6-3, Ronaldo alianza kwenye benchi na hakucheza hata dakika moja.

Muhtasari

• Kocha wa United Eric Ten Hag alisutwa vikali kwa kutomchezesha Ronaldo kwenye mechi hiyo kubwa ya debi.

Wikendi kulikuwepo na mechi kubwa ya debi ya jiji la Manchester nchini Uingereza ambapo mahasimu wa siku za hivi karibuni United na City walikuwa wanamenyana katika ligi kuu ya Premia.

Katika mechi hiyo, timu ya Manchester City iliinyika Manchester United kibano cha mabao 6 kwa matatu na mechi hiyo imezungumziwa sana, haswa kutokana na tukio kubwa la mchezaji nguli Christiano Ronaldo kuanza akiwa ameketi kwenye benchi.

Video moja ambayo ilipakiwa na shirika la habari la Sky Sports kwenye Tweeter inaonesha jinsi mchezaji huyo alikuwa akihisi mara baada ya timu yake kulimwa mabao manne bila jibu katika kipindi cha kwanza, akiwa kwenye benchi licha ya ukali na uwezo mkubwa alio nao wa kuisaidia timu yake katika kufunga mabao.

Video hiyo ambayo sasa ni gumzo la mitandaoni ilimuonesha Ronaldo akiinamisha uso kwa hisia cha uchungu kutokana na kunyimwa nafasi ya kuingia uwanjani kucheza huku timu yake ikizidi kuzamishwa kwa mabao kama mvua ya gharika hadi sita.

Mabaa ya City yalifungwa na wachezaji wawili tu, Phil Foden na mshambuliaji hatari Erling Halland ambao kila mmoja alijinyakulia mpira kwa kufunga mabao matatu, kwa kimombo Hattrick.

Kocha mkuu Erick Ten Hag alimaliza kuwaingiza wachezaji wake wa akiba wote watano uwanjani kipindi cha pili pasi na kumuingiza Ronaldo na kamera zilimuonesha mchezaji huyo akiwa amesawijika uso kweli kweli kwa kutoamini kilichokuwa kinaendelea uwanjani.

Tukio la kocha kutomchezesha Ronaldo kwenye mechi kubwa kama ile lilipokelewa kwa njia mbali mbali na baadhi ya wachezaji wakongwe na wachanganuzi wa soka ambao walisema kutomchezesha mchezaji huyo ni kama kumkosea heshima haswa kwa kuangalia mchango wake mkubwa kwenye klabu.