(+video) "Ameisha" Mashabiki wahofia baada ya Ronaldo kupoteza nafasi ya wazi Vs Omonia

United walitoka nyuma na kupata ushindi finyu dhidi ya Omonia kwa mabao 3-2

Muhtasari

• "Inasikitisha kuona toleo hili la Ronaldo, si yule tunayemjua tangu zamani" shabiki mwingine alisema.

Alhamis usiku huwa ni siku ya wapenzi wa mchezo wa soka kujifurahisha, haswa wakati wa ligi ya Uropa.

Timu ya Manchester United Alhamis usiku ilikuwa inamenyana na timu ya Omonia. Katika mechi hiyo ambayo United waling’ang’ana dhidi ya malimbukeni hao hadi kuibuka washindi dakika za mwisho, gumzo kubwa lilikuwa ni mchezaji nguli kwa muda mrefu, Christiano Ronaldo.

Katika video ambazo zimekuwa zikisambazwa kwenye mtandao wa Tweeter, Ronaldo amekuwa akisutwa baada ya kuonekana akishindwa kufunga bao la wazi kabisa.

Ronaldo alionekana kubaki moja kwa moja na mlinda lango wa Omonia ila katika tukio lisolo la kawaida, mchezaji huyo alikosa kutikiza wavu, jambo ambalo wengi wamesema si kawaida yake kabisa.

Mashabiki waliokuwa wakimsema vibaya kocha mkuu Eric Ten Hag angalau walipumua na kuonekana kukubaliana na maamuzi yake ya kutomchezesha mshambuliaji huyo wa kimataifa kutoka Ureno.

Walimkejeli Ronaldo kuwa huenda ni kweli amefikia kikomo cha ubora wake katika ulimwengu wa soka na wengine kumtaka kustaafu kabla hajalipaka jina lake tope.

Nafasi kubwa ya kufunga ilikuja zikiwa zimesalia dakika 15 mpira kumalizika ambapo alikabidhiwa pasi moja maridadi kutoka kwa umbali wa yadi nane. Hata hivyo, Ronaldo hakuweza kulenga shabaha kwani juhudi zake zilifuma nguzo ya lango na kupoteza nafasi hiyo kumemkaribishia masimango mengi kutoka kwa mashabiki.

“Nilikuwa namtetea Ronaldo, lakini sivyo tena. Naofia kusema kwamba mchezaji huyu ameisha kabisa,” Mmoja aliandika.

“Inasikitisha kuona toleo hili la Ronaldo, si yule tunayemjua tangu zamani,” shabiki wa muda mrefu alionesha sikitiko lake.