(+video) Conte ashindwa kuzuia machozi akimkumbuka marehemu kocha wa mazoezi wa Spurs

Kocha wa mazoezi Gian Piero Ventrone alifariki wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 61.

Muhtasari

• Katika video ambayo inazidi kusambazwa mitandaoni, Conte alionekana kuzidiwa na hisia huku machozi yakimtiririka pasi na kupenda kwake.

• Conte wamekuwa wakifanya kazi na Ventrone kwa muda mrefu tangu enzi zake kama kocha wa Juventus.

Wiki hii mashabiki na wakereketwa wa ligi kuu ya Premia nchini Uingereza walipigwa na butwaa kufuatia kifo cha kocha wa mazoezi ya mwili wa timu ya Tottenham Hotspurs, Gian Piero Ventrone akiwa na umri wa miaka 61.

Ventrone mpaka kufa kwake alikuwa ni rafiki wa karibu sana wa kocha mkuu wa timu hiyo Muitaliano Antonio Conte. Inaarifiwa kwamba wawili hao waliwahi fanya kazi pamoja Conte akiwa mkufunzi wa timu ya Juventus na pia wakaungana kwa mara nyingine tena nchini Uingereza katika timu ya Tottenham.

Jumamosi timu hiyo ilikuwa inacheza mechi ya ugenini dhidi ya Brighton & Hoven ambapo heshima za dakika moja zilizotelwa kwa ajili ya marehemu Ventrone, huku wachezaji, mashabiki na waamuzi wakisimama tisiti na kuonesha heshima zao za mwisho kwa ishara ya kumpigia makofi Ventrone.

Bila shaka ilikuwa ni dakika moja yenye hisia za kuumiza sana si tu mashabiki bali hata wachezaji na kocha Conte ambaye walikuwa wametangamana sana na marehemu.

Katika video ambayo inazidi kusambazwa mitandaoni, Conte alionekana kuzidiwa na hisia kabisa mpaka kushindwa kuzuia machozi ambayo yalionekana kumtiririka wazi wazi.

Kabla ya mchezo huo, meneja Conte alisema ilikuwa ngumu kuamini kwamba Ventrone hayupo tena.

"Kutafuta maneno kwa Gian Piero ni ngumu sana wakati huu. Kwa kweli tumehuzunishwa na uchungu wa kile kilichotokea. Pia kwa sababu hakuna mtu aliyetarajia hali hii. Lakini wakati mwingine unajua maisha sio hali nzuri kila wakati,” Conte alisema huku akijikakamua kuzuia machozi.

Mechi hiyo ilimalizika kwa faida ya Spurs ambao waliwalemea Brighton kwa bao moja liilofungwa na mchezaji matata Harry Kane.