MAKAO MAPYA

Mshambuliaji wa zamani wa Gor Mahia atua Zambia

Onyango alisema kocha mkuu wa Gor Mahia alimwambia hayuko katika mipango yake ya siku za usoni.

Muhtasari

•Akizungumza awali, Onyango alithibitisha kwamba McKinistry alikuwa amemjulisha kuwa hakuwa sehemu ya mipango yake.

•Onyango anaungana na kiungo wa kati wa Uganda Hashim Sempala, mchezaji mwenzake wa zamani wa Gor Mahia

Samuel Onyango
Samuel Onyango
Image: HISANI

Mshambuliaji wa zamani wa Gor Mahia, Samuel Onyango, huenda akatambulishwa na timu ya Ligi Kuu ya Zambia, Kabwe Warriors, kama mchezaji wao mpya wakati wowote wiki hii.

Onyango alifunga safari kuelekea Zambia mapema wiki jana kukamilisha uhamisho wa kujiunga na timu hiyo.

Fowadi huyo wa Harambee Stars aliachiliwa na kocha wa Gor Mahia Johnathan McKinistry wiki mbili zilizopita na hakuwa miongoni mwa wachezaji waliotambulishwa rasmi wakati wa makubaliano ya ufadhili kati ya klabu hiyo na Sportpesa mwezi mmoja uliopita.

Mtaalamu huyo raia wa Ireland alisema atatafuta mshambuliaji anayefaa kuchukua nafasi ya Onyango miongoni mwa wachezaji aliowapandisha hivi karibuni kutoka timu ya vijana.

Onyango alisaini mkataba wa muda mrefu na Gor Mahia mnamo Novemba 2017 kutoka kwa wapinzani wao Ulinzi Stars na kufanikiwa kutwaa mataji matatu mfululizo ya ligi kuu akiwa na klabu hiyo katika misimu ya 2017/18, 2018/19 na 2019/20.

Akizungumza awali, Onyango alithibitisha kwamba McKinistry alikuwa amemjulisha kuwa hakuwa sehemu ya mipango yake na klabu haikuwa na nia ya kuongeza mkataba wake ambao ulikuwa unamalizika Novemba.

Akiwa Kabwe Warriors, anatarajiwa kuingia kwenye viatu vya fowadi wa zamani wa AFC Leopards na Kariobangi Sharks, Harrison Mwendwa aliyejiunga na Singida Big Stars nchini Tanzania Julai.

Onyango anaungana na kiungo wa kati wa Uganda Hashim Sempala, mchezaji mwenzake wa zamani wa Gor Mahia.