BASHASHA

Martial arejea kikosini kwa kishindo

Mfaransa huyo alikabiliwa na changamoto nyingi mwanzoni mwa msimu, ikiwa ni pamoja na kuzorota kwa utimamu wa mwili.

Muhtasari

•Hata hivyo, aliweka vikwazo hivyo kando na kufanikiwa kumvutia meneja mpya wa Manchester United Erik ten Hag katika mechi zao za maandalizi.

•Hatima yake huko United iliegemea kwa Ten Hag, ambaye anaonekana kuwa shabiki wa fowadi huyo na Martial amerudisha imani kwa kufanya vyema hadi sasa.

Anthony Martial
Anthony Martial
Image: HISANI

Marcus Rashford amemsifu Anthony Martial kwa kurejea uwanjani kwa kishindo baada ya kukumbwa na jeraha siku za nyuma.

Mfaransa huyo alikabiliwa na changamoto nyingi mwanzoni mwa msimu, ikiwa ni pamoja na kuzorota kwa utimamu wa mwili.

Hata hivyo, aliweka vikwazo hivyo kando na kufanikiwa kumvutia meneja mpya wa Manchester United Erik ten Hag katika mechi zao za maandalizi.

Martial aliingia akitokea benchi na kufunga mabao mawili katika mchezo wao wa derby dhidi ya Manchester City kabla ya kuongeza jina lake kwenye ukurasa wa mabao tena katika mechi yao ya Ligi ya Europa dhidi ya Omonia huko Cyprus siku chache baadaye.

Martial, 26, atakuwa akipigania nafasi katika kikosi cha kwanza na Rashford aliyefunga mara mbili dhidi ya Omonia.

Licha ya hilo, Rashford amesema ni uamuzi mzuri kwa United kumrejesha timuni mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa.

"Yeye ni mchezaji mkubwa kwetu ambaye amekuwa kikosini kwa muda mrefu sasa. Sote wawili tumewahi kukumbwa na majeraha, kwa hivyo ni vizuri kwake kupata dakika na kufanya matokeo."

Hatua hii ni afueni kubwa kwa Martial ambaye hapo awali alikumbwa na msimu mgumu huko United na hata alitumia kipindi chote cha pili cha msimu uliopita kwa mkopo huko Seville Uhispania ambapo pia alishindwa kutamba.

Hatima yake huko United iliegemea kwa Ten Hag, ambaye anaonekana kuwa shabiki wa fowadi huyo na Martial amerudisha imani kwa kufanya vyema hadi sasa.