UWEZO WA KIUFUNDI

Kocha wa Manchester United Ten Hag amsifu Antony

Antony dos Santos alifuta juhudi za Alex Iwobi aliyewaweka Everton kifua mbele mwanzoni mwa kipindi cha kwanza.

Muhtasari

•Ten Hag aliwaambia waandishi wa habari kwamba alifurahishwa sio tu na uwezo wa mchezaji huyo wa kushambulia na kufunga mabao, bali pia uimara wake katika ulinzi.

•Ten Hag na Antony wamewahi kufanya kazi pamoja katika klabu ya Uholanzi ya Ajax huko Amsterdam.

Wachezaji wa Manchester United wampongeza Antony baada ya kutikisa wavu
Wachezaji wa Manchester United wampongeza Antony baada ya kutikisa wavu
Image: HISANI

Meneja wa Manchester United Erik ten Hag amesema fowadi wa Brazil Antony Matheus dos Santos tayari amedhibitisha uwezo wake katika mechi alizochezea klabu hiyo hadi sasa.

Ten Hag alimmiminia sifa winga huyo ambaye aliweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza wa klabu hiyo kufunga bao katika mechi zake tatu za kwanza za Ligi Kuu.

Antony alitikisa wavu dakika ya 15 na kufuta bao la ufunguzi la Everton kabla ya Cristiano Ronaldo kufunga bao lake la 700 katika ngazi ya klabu mwishoni mwa kipindi cha kwanza lilopatia Manchester United ushindi wa 2-1.

Ten Hag aliwaambia waandishi wa habari kwamba alifurahishwa sio tu na uwezo wa mchezaji huyo wa kushambulia na kufunga mabao, bali pia uimara wake katika ulinzi.

“Tunapaswa kutarajia zaidi kutoka kwake. Anahitaji changamoto, ndiyo maana alikuja Ligi Kuu na anaipata hapa. Anataka kucheza na wachezaji bora,” alisema meneja huyo.

“Kuanzia hapo atapiga hatua na ndivyo unavyoona katika wiki ya kwanza alikuwa akifunga mabao na amefanya mambo mazuri. Lakini pia naona nafasi kubwa ya kuboresha mchezo wake.

Ten Hag alisema licha ya uwezo wa kipekee wa kiufundi wa Antony, anahitaji kufanya mabadiliko zaidi.

“Katika mchezo wa kwanza hakuwa na busara katika kulinda lakini safari hii alikuwa mzuri sana, alikuwa na nidhamu ya kweli na alikuwa na nafasi nzuri”

Ten Hag na Antony wamewahi kufanya kazi pamoja katika klabu ya Uholanzi ya Ajax huko Amsterdam.

“Anaweza kwenda pande zote mbili kwa miguu yote miwili. Anapaswa kufanyia kazi hatua hiyo,” alisema meneja huyo.

“Tayari tulifanya hivyo huko Amsterdam pamoja naye, tukifanyia kazi hilo. Anaweza kuvuka kwa mguu wake wa kulia pia lakini ni mchezaji mdogo ambaye tunapaswa kumkuza na anatakiwa kujiendeleza pia.”