Mo Salah avunja rekodi ya hat trick ya haraka zaidi kwenye Champions League

Pia aliibuka mchezaji aliyefungia klabu moja ya Uingereza mabao mengi katika Champions League.

Muhtasari

•Mabao saba ya The Reds yalifungwa na washambulizi Roberto Firmino (2), Darwin Nunez (1), Mohammed Salah (3) na Harvey Elliot (1). 

•Mabao ya mshambulizi huyo wa Misri yalikuja katika dakika ya 75, 80 na 81. 

Raia huyo wa Misri amevunja rekodi ya hat trick ya haraka zaidi kwenye Champions League.
Mshambulizi Mo Salah. Raia huyo wa Misri amevunja rekodi ya hat trick ya haraka zaidi kwenye Champions League.
Image: TWITTER// LIVERPOOL

Jumatano usiku klabu ya Liverpool ilipata ushindi mkubwa wa 7-1 dhidi ya Rangers katika mechi yao ya nne ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2022/23.

Mabao saba ya The Reds yalifungwa na washambulizi Roberto Firmino (2), Darwin Nunez (1), Mohammed Salah (3) na Harvey Elliot (1). Kiungo wa kati wa Canada Scott Arfield alifungia Rangers bao la pekee katika dakika ya 17.

Katika mechi hiyo, Mo Salah alivunja rekodi ya hat trick kwenye Champion League kwa kufunga mabao matatu ya haraka zaidi katika mechi moja.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri ambaye aliingia uwanjani katika kipindi cha pili, dakika ya 68 alifunga mabao hayo chini ya dakika sita tu. Mabao hayo yake yalikuja katika dakika ya 75, 80 na 81. 

Licha ya Mo Salah kufunga hat trick katika mechi hiyo, Roberto Firmino wa Brazil ambaye alifunga mabao mawili katika dakika ya 24 na 55 ndiye aliyeshinda tuzo la mchezaji bora wa mechi kwa ubabe ambao alionyesha ugani Ibrox.

Mo Salah pia alivunja rekodi nyingine usiku wa Jumatano huku akiibuka mchezaji aliyefungia klabu moja ya Uingereza mabao mengi katika Champions League. Kufikia sasa amefungia Liverpool mabao 38 kwenye mashindano ya kombe hilo ambalo linathaminiwa na kuheshimika sana barani Ulaya.

Kwa sasa Liverpool imekalia nafasi ya pili katika kundi A ya Champions League 2022/23 huku mechi nne zikiwa zimechezwa tayari. Napoli ambayo haijapoteza mechi yoyote kufikia sasa imeongoza kundi hilo kwa pointi 12, tatu mbelel ya vijana wa Jurgen Klopp huku Ajax na Rangers zikichukua nafasi ya tatu na ya nne kwa pointi tatu na sufuri mtawalia.