Good Ebening! Aliyekuwa kocha wa Arsenal, Unai Emery arejea EPL

Aston Villa imemteua Unai Emery kuwa Kocha Mkuu mpya kufuatia kutimuliwa kwa Steven Gerrard.

Muhtasari

•Villa ilithibitisha uteuzi wa kocha huyo wa zamani wa Arsenal Jumatatu jioni kupitia tovuti rasmi ya klabu.

•Gerrard alifutwa kazi Alhamisi wiki jana, masaa machache tu baada ya kupokea kichapo cha 3-0 kutoka kwa Fulham.

.Aliyekuwa kocha wa Arsenal ameteuliwa kama kocha mkuu wa Aston Villa
Unai Emery .Aliyekuwa kocha wa Arsenal ameteuliwa kama kocha mkuu wa Aston Villa
Image: HISANI

Klabu ya Aston Villa imemteua Unai Emery kuwa Kocha Mkuu mpya kufuatia kutimuliwa kwa Steven Gerrard.

Villa ilithibitisha uteuzi wa kocha huyo wa zamani wa Arsenal Jumatatu jioni kupitia tovuti rasmi ya klabu.

"Aston Villa inafuraha kutangaza uteuzi wa Unai Emery kama Kocha Mkuu mpya wa klabu," taarifa ya klabu ilisoma.

Raia huyo wa Uhispania ambaye amekuwa akihudumu kama kocha wa Villareal katika kipindi cha takriban miaka miwili iliyopita ataanza majukumu yake mapya katika klabu ya Aston Villa mwezi ujao. 

Uteuzi wa mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 50 unajiri siku chache tu baada ya klabu hiyo kumtimua aliyekuwa mchezaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uingereza, Steven Gerrard kama kocha mkuu.

Gerrard alifutwa kazi Alhamisi wiki jana, masaa machache tu baada ya kupokea kichapo cha 3-0 kutoka kwa Fulham. Kabla ya kufutwa kwake, kiungo wa kati huyo wa zamani alikuwa ameandikisha matokeo hafifu na klabu hiyo ya jiji la Birmingham na kuiacha katika nafasi ya 17 kwenye jedwali.

Kabla ya kujiunga na Villareal, Unai Emery aliwahi kufanya kazi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) akihudumu kama kocha wa Arsenal kati ya 2018 na 2019. Alitimulia Novemba 2019 kufuatia matokeo hafifu.

Katika kipindi chake na Wanabunduki aliweza kuwafikisha hadi fainali ya Europa League ambapo walipoteza kwa Chelsea.

Emery anakumbukwa zaidi na mashabiki wa Ligi Kuu kwa salamu zake maarufu 'Good Ebening' ambazo zilimfanya akejeliwe sana.