Unai Emery aanza kazi rasmi kama kocha mkuu wa Aston Villa

Kocha huyo ameanza kazi baada ya kupata kibali alichokuwa amesubiri.

Muhtasari

•Unai aliwasili Bodymoor Heath Jumanne jioni na alikuwa akingojea kibali chake cha Visa ili kuanza mazoezi na klabu yake mpya.

•Aston Villa ilimsajili Unai kama kocha mkuu mpya wiki jana, siku chache tu baada ya kumpiga kalamu Steven Gerrard.

Unai Emery ameanza kazi rasmi katika Aston Villa
Image: TWITTER// ASTON VILLA

Unai Emery ameanza rasmi kazi yake kama kocha mkuu wa klabu ya Aston Villa.

Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 50 aliwasili Bodymoor Heath Jumanne jioni na alikuwa akingojea kibali chake cha Visa ili kuanza mazoezi na klabu yake mpya.

Siku ya Jumatano, Aston Villa ilitangaza kuwa meneja huyo wa zamani wa Arsenal tayari ameanza kazi baada ya kupata kibali alichokuwa amesubiri.

"Tuende kazi @UnaiEmery," klabu hiyo iliandika chini ya video ya mkufunzi huyo akiwa katika uwanja wa mazoezi.

Aston Villa ilimsajili Unai kama kocha mkuu mpya wiki jana, siku chache tu baada ya kumpiga kalamu Steven Gerrard.

"Aston Villa inafuraha kutangaza uteuzi wa Unai Emery kama Kocha Mkuu mpya wa klabu," taarifa ya klabu ilisoma.

Raia huyo wa Uhispania ambaye alikuwa akihudumu kama kocha mkuu wa Villareal katika kipindi cha takriban miaka miwili iliyopita alirejea katika Ligi Kuu takriban miaka miwili baada ya kuondoka.

Uteuzi wa mkufunzi huyo ulijiri siku chache tu baada ya klabu hiyo kumtimua aliyekuwa mchezaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uingereza, Steven Gerrard kama kocha mkuu.

Gerrard alifutwa kazi takriban wiki mbili zilizopita, masaa machache tu baada ya kupokea kichapo cha 3-0 kutoka kwa Fulham. Kabla ya kufutwa kwake, kiungo wa kati huyo wa zamani alikuwa ameandikisha matokeo hafifu na klabu hiyo ya jiji la Birmingham na kuiacha katika nafasi ya 17 kwenye jedwali.

Kabla ya kujiunga na Villareal, Unai Emery aliwahi kufanya kazi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) akihudumu kama kocha wa Arsenal kati ya 2018 na 2019. Alitimulia Novemba 2019 kufuatia matokeo hafifu.

Katika kipindi chake na Wanabunduki aliweza kuwafikisha hadi fainali ya Europa League ambapo walipoteza kwa Chelsea.