Mfanyikazi wa Manchester City aonekana na tattoo ya Manchester United

Timu hizo mbili ni mahasimu wa jadi ambao wanataniana kwa jina la kimajazi la 'Majirani wenye Kelele'

Muhtasari

• Ingawa hakuna ubaya kwa Man City kuajiri shabiki wa United, bila shaka mkaguzi huyo wa uwanja huenda atajipata katika chuki kali kutoka kwa mashabiki wa Man City.

Shabiki wa Man U ambaye ni mfanyikazi wa Man City.
Shabiki wa Man U ambaye ni mfanyikazi wa Man City.
Image: Maktaba, The Sun

Unaambiwa maadui pamoja na washindani wako ndio mashabiki wako wakubwa! Kweli, hili linadhihirika baada ya mfanyikazi wa timu ya Manchester City ya nchini Uingereza kuonekana akiwa na mchoro wa tattoo ya watani wao Manchester United mguuni.

Katika picha hiyo ambayo ilisambazwa pakubwa, mfanyikazi huyo wa uwanjani alionekana akiwa amevalia bukta fupi na soksi zilizokuwa hazijafika kwenye muundi akiwa uwanjani kwa matayarisho ya uwanja kwa minajili ya mechi baina ya mabingwa hao watetezi wa EPL na Fulham.

Kamera zilimpiga picha kwenye muundi wake akiwa amechorwa tattoo ya Man U jambo ambalo limezua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii, baadhi wakisema kuwa ushabiki ni tofauti na kibarua.

Ingawa hakuna ubaya kwa Man City kuajiri shabiki wa United, bila shaka mkaguzi huyo wa uwanja huenda atajipata katika chuki kali kutoka kwa mashabiki wa Man City ambao ni watani wa jadi wa Man U wanaotaniana kwa jina, ‘Majirani wenye kelele’

Hata hivyo, mechi ya City dhidi ya Fulham ilikamilika kwa ukakasi mkubwa huku City wakipata bao la ushindi dakika za zima taa tulale kupitia mkwaju wa penalti uliotiwa kinywani na mshambuliaji matata Earling Halaand.

Julian Alvarez aliifungia City bao la kwanza dakika ya 16 kabla ya Andreas Pereira kulifuta kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika. Mechi hiyo ilionekana kuisha kwa wenyeji sare ya 1-1 kabla ya Kevin De Bruyne kushinda penalty hiyo ambayo Halaand alizamisha wavuni.