Napenda Arsenal, natamani washinde ligi msimu huu - Ronaldo

Napenda kocha wao na nadhani wana timu nzuri sana - Ronaldo alisema.

Muhtasari

• Kwa sasa, Arsenal wanaongoza msimamo wa ligi kuu ya EPL wakiwa pointi tano mbele ya Manchester City ambao wanashikilia nafasi ya pili.

Ronaldo aisifia Arsenal
Ronaldo aisifia Arsenal
Image: Maktaba

Mchezaji Christiano Ronaldo kwa mara ya kwanza amemwaga moyo wake wa upendo kwa timu ya Arsenal na kusema kwamba atajihisi mwenye faraja kuu iwapo miamba hao wa kutoka London watashinda ubingwa wa EPL msimu huu.

Katika mwendelezo wa mahojiano yake na mwanahabari mwenye utata, Piers Morgan, Ronaldo alisema kwamab anaipenda sana Arsenal pamoja na uongozi wake na kuwa iwapo watanyakuwa ubingwa wa premia basi atakuwa amefarijika zaidi.

“Natamani Arsenal washinda ligi kuu ya Premia kama si Manchester United. Nitajihisi mwenye furaha tele endapo Arsenal watalichukua taji nyumbani. Napenda kocha wao na nadhani wana timu nzuri sana,” Ronaldo alimwambia Morgan.

Katika sehemu ya kwanza ya mahojiano hayo awali, Ronaldo alikejeli uongozi wa timu yake ya Manchester United akisema kwamba wamebaki nyuma katika kila kitu na wala hawataki kukumbatia mambo mapya ya kitekinolojia ambayo yamekumbatiwa na timu zingine Ulaya.

Pia aliwakosoa wachezaji wenzake walioshiriki pamoja uwanjani akiwemo Wyne Rooney kwa kumkejeli vibaya.

Baada ya mahojiano hayo ya moto ambayo yalizua gumzo kubwa kote duniani mapema wiki hii, uongozi wa United ulisema ulikuwa ukutane katika kikao cha dharura ili kujadili mustakabali wao na Ronaldo klabuni hapo, haswa baada ya kuonekana kutoa matamshi yanayolenga klabu kwa njia hasi.

Alhamisi tulikutaariu kuwa picha kubwa ya kiungo mshambulizi huyo iliondolewa katika uwanja wa Manchester United katika kile ambacho baadhi walihisi ndio mwanzo wanavunja ukuruba wao naye huku wengine wakisema ni uwanja kufanyiwa maandalizi kwa ajili ya kipute cha raga kitakachoandaliwa ugani Old Trafford.

Kwa sasa, Arsenal wanaongoza msimamo wa ligi kuu ya EPL wakiwa pointi tano mbele ya Manchester City ambao wanashikilia nafasi ya pili.