(video) Wachezaji wageuza uwanja kuwa ulingo wa ngumi, refa atoa kadi 6 nyekundu

Watu kadhaa kutoka pande zote mbili wakiwemo wachezaji wa akiba na benchi la kiufundi waliruka uwanjani na kuanza kupigana.

Muhtasari

• Katika mechi hiyo kali iliyochezwa Jumapili, Tukio hilo lilitokea katika muda wa kumalizika kwa mechi.

Mechi kati ya Zenit St Petersburg na Spatark Moscow nchini Urusi iligeuka kuwa karaha baada ya wachezaji kutoka pande zote mbili kushambuliana hadharani na kuzua vita vikali uwanjani.

Katika mechi hiyo kali iliyochezwa Jumapili, Tukio hilo lilitokea katika muda wa kumalizika kwa mechi na lilichochewa na Quincy Promes na William Barros. Mwamuzi Vladimir Moskalev alijaribu kupunguza mzozo kati ya wachezaji hao wawili, lakini ilikuwa ni kuchelewa sana.

Baada ya kulemewa na maguvu ya wachezaji hao wote waliojawa na ghadhabu na hasira, refa Moskalev alilazimika kuzama mfukoni mara sita na kutoa kadi nyekundu ambazo ziliwaramba wachezaji 6 kutoka timu zote mbili.

Watu kadhaa kutoka pande zote mbili wakiwemo wachezaji wa akiba na benchi la kiufundi waliruka uwanjani na katika video hiyo, mwamuzi Moskalev anaonekana akijaribu kutuliza hali bila mafanikio hata kidogo.

Sports Breif Kenya waliripoti kuwa kadi zote 6 nyekundu zilitolewa kwa wachezaji wa akiba walioingia uwanjani na kuchochea fujo hiyo hata zaidi.

Mchezo huo ulitoka sare ya 0-0 wakati wa mtanange huo. Baada ya utaratibu kurejeshwa, mchezo ulianza tena, na Zenit kushinda mchezo kupitia mikwaju ya penalti baada ya mechi ili kusonga mbele kwa raundi inayofuata.

Kwingineko nchini Uturuki hali kama hiyo ilishuhudiwa ambapo mashabiki walishambuliana na baadae ambulesi ilipokuwa ikimhudumia shabiki mmoja, jamaa alionekana akikimbia na kibendera cha kona kabla ya kumshambulia golikipa wa timu ya ugenini.

Vyombo vya habari viliripoti kuwa golikipa huyo alipata majeraha mabaya ya kichwa yaliyolazimu kukimbizwa hospitalini kwa dharura.