Wanyama akubali kurejea Harambee Stars mwaka mmoja baada ya kustaafu

Namwamba atarejea kikamilifu kwenye kikosi cha taifa kufuatia mazungumzo yao.

Muhtasari

•Ababu alidokeza kuwa mchezaji huyo wa CF Montreal atarejea kikamilifu kwenye kikosi cha taifa kufuatia mazungumzo yao.

•Ababu aliwahimiza wachezaji Wakenya kukumbatia mabadiliko yanayofanywa kwa lengo la kufufua sekta ya soka nchini.

Mchezaji wa Harambee Stars Victor Wanyama na Waziri Ababu Namwamba
Image: TWITTER// ABABU NAMWAMBA

Kiungo wa kati Victor Mugubi Wanyama amekubali kurudi kwenye timu ya taifa ya Harambee Stars, takriban mwaka mmoja baada ya kustaafu kutoka soka ya kimataifa.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi asubuhi, Waziri wa Masuala ya vijana, Michezo na Sanaa Ababu Namwamba alidokeza kuwa mchezaji huyo wa CF Montreal atarejea kikamilifu kwenye kikosi cha taifa kufuatia mazungumzo yao.

"Nimefurahia kuwa Victor Wanyama amekubali kurejea kikamilifu Harambee Stars, na kubatilisha uamuzi wake wa awali wa kujiondoa kwenye timu hiyo," Namwamba alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Waziri huyo aliambatanisha ujumbe huo na picha yake akiwa katika kikao na Wanyama pamoja na wasimamizi wake.

Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wachezaji Wakenya kukumbatia mabadiliko yanayofanywa kwa lengo la kufufua sekta ya soka nchini.

"Katika dhamira yetu ya kujenga upya soka letu na kuinua timu zetu za taifa, wachezaji wetu wakuu lazima wawe kiini cha mwamko huu. Ogada Olunga pia yumo ndani," alisema.

Upande wake,Wanyama alifichua kuwa alijadialana masuala ya soka nchini na waziri huyo na kueleza kuridhishwa kwake na mikakati ambayo serikali imeweka katika juhudi za kuinua sekta ya michezo.

"Leo nimemtembelea waziri wa Michezo. Tulijadili hali ya sasa ya michezo na hasa soka nchini. Nimefurahishwa na mipango ambayo serikali imeweka ili kuinua hali ya soka nchini.

Pia tulibadilishana mawazo kuhusu jinsi ya kuboresha mchezo katika maeneo yote nchini Kenya. Jukumu ni kufanya kazi pamoja na kupeleka soka katika ngazi nyingine. Nimefurahishwa na kile kilicho mbele, " Wanyama alisema.

Wanyama alitangaza kujiondoa kwenye timu ya Taifa Harambee Stars mwezi Septemba 2021. Alikuwa nahodha tangu 2013 alipochukua nafasi ya Dennis Oliech.

“Siku zote ilikuwa ndoto yangu kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi yangu, kwa kujivunia sana naweza kusema nimepata bahati ya kuishi ndoto yangu.

"Tangu kucheza mechi yangu ya kwanza dhidi ya Nigeria hadi kuwa nahodha wa timu kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Misri, miaka hii 14 imepita ni zaidi ya nilivyowahi kufikiria.

"Tumekuwa na nyakati nzuri pamoja na ninajivunia kuwa nahodha na kiongozi wenu.

Lakini mambo yote mazuri lazima yafike mwisho hatimaye; na baada ya kufikiria kwa muda mrefu, nimefanya uamuzi mgumu sana wa kustaafu soka ya kimataifa,” alisema kiungo huyo wa kati katika taarifa aliyoiweka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.