Kwa nini Ronaldo aliondoka uwanjani akilia? Mchezaji huyo ajibu kwa hisia

"Mengi yamesemwa, mengi yameandikwa, mengi yamekisiwa, lakini kujitolea kwangu kwa Ureno hakubadiliki."

Muhtasari

• Siku zote nilikuwa mmoja nikipigania lengo la wote na singewahi kuwapa kisogo wenzangu na nchi yangu - Ronaldo alisema.

• Ureno walibanduliwa katika mechi ya robo fainali na Morocco kwa kufungwa bao moja bila jibu.

Ronaldo alia baada ya Ureno kubanduliwa kombe la dunia
Ronaldo alia baada ya Ureno kubanduliwa kombe la dunia
Image: Facebook

Nyota wa Ureno Christiano Ronaldo kwa mara ya kwanza amevunja kimya chake tangu timu yake kuondolewa katika mashindano ya kombe la dunia na Morocco.

Ureno ilibanduliwa nje ya mashindano hayo katika mechi ya kufuzu nusu fainali na Ronaldo aliingia kama mchezaji wa akiba lakini hakuweza kusaidia timu yake kufuta bao la Morocco ambalo lilisimama mpaka kipenga cha mwisho.

Pindi tu baada ya mechi hiyo kukamilika, Ronaldo alionekana akitoka nje ya uwanja huku akilia kwa uchungu kwani hakuweza kuamini ndoto yake ya kuongeza medali ya kombe la dunia kwenye rafu yake imemtoka hivyo tu – kumbuka haya ndio mashindano ya kombe la dunia ya mwisho katika taaluma ya mchezaji huyo nguli.

Kupitia ujumbe ambao aliachia kwenye kurasa zake za mitandaoni, Ronaldo alisema kuwa kwa miaka 16 iliyopita, ilikuwa ni ndoto yake kuitumikia Ureno akitumai kuisaidia kushinda kombe la dunia lakini sasa ndoto hiyo imeumbuka.

“Kushinda Kombe la Dunia kwa Ureno ilikuwa ndoto kubwa na kabambe ya maisha yangu. Nilipigania. Nilipigania sana ndoto hii. Katika mechi 5 nilizofunga kwenye Kombe la Dunia kwa zaidi ya miaka 16, kila mara nikiwa na wachezaji wazuri na kuungwa mkono na mamilioni ya Wareno, nilijitolea kwa kila kitu. Acha yote nje ya uwanja. Sikuwahi kugeuza uso wangu kwenye pambano na sikukata tamaa juu ya ndoto hiyo. Cha kusikitisha jana ndoto iliisha,” Ronaldo alisema.

Pia alisema kuwa katika siku za hivi karibuni, amekuwa akisemwa kwa mabaya na mazuri jambo ambalo halijamshtua ila linauma sana kuona anageuzwa kubebeshwa lawama katika kila baya ambalo linatokea huku atu wakisahau mazuri ambayo amefanya katika tasnia ya soka kwa miaka zaidi ya 20.

“Sio thamani ya kukabiliana na joto. Nataka tu mfahamu kwamba mengi yamesemwa, mengi yameandikwa, mengi yamekisiwa, lakini kujitolea kwangu kwa Ureno hakubadiliki hata kidogo. Siku zote nilikuwa mmoja nikipigania lengo la wote na singewahi kuwapa kisogo wenzangu na nchi yangu. Si mengi zaidi ya kusema kwa sasa. Asante Ureno. Asante Qatar Ndoto ilikuwa nzuri wakati ilidumu,” Mreno huyo alisema kwa hisia.