Sakaja awaalika Wakenya kutazama fainali za Kombe la Dunia katika uwanja wa Uhuru Park

Katika taarifa yake Jumapili, Sakaja alisema kutakuwa na fataki za ajabu baada ya mechi.

Muhtasari
  • Siku ya Jumatatu, Sakaja alizindua rasmi Tamasha la Nairobi, 2022
  • Tukio hilo la siku sita ambalo linakaribia kukamilika lilishuhudia wakazi wa Nairobi wakiburudika na kudhihirisha utamaduni wa Nairobi
Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja
Gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja
Image: Facebook

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amewaalika wakazi wa Nairobi kuhudhuria Tamasha la Nairobi na kutazama mechi ya mwisho ya Kombe la Dunia katika bustani ya Uhuru.

Mechi kati ya Ufaransa na Argentina itachezwa Jumapili saa kumi na mbili jioni.

Katika taarifa yake Jumapili, Sakaja alisema kutakuwa na fataki za ajabu baada ya mechi.

"Njoo tutazame fainali za Kombe la Dunia pamoja katika uwanja wa Uhuru Park tunapofunga tamasha la Nairobi. Fataki za ajabu huonyeshwa baada ya tuzo za Nganya, mti wa Krismasi na usaidizi kwa nyumba 40 za watoto kwa msimu wa sikukuu,” alisema.

Siku ya Jumatatu, Sakaja alizindua rasmi Tamasha la Nairobi, 2022.

Tukio hilo la siku sita ambalo linakaribia kukamilika lilishuhudia wakazi wa Nairobi wakiburudika na kudhihirisha utamaduni wa Nairobi.

Akizungumza wakati wa sherehe za 59 za Jamhuri katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo, Sakaja alisema tamasha hilo litatoa fursa kwa Wakenya kuthamini vyakula, tamaduni na sanaa mbalimbali za jiji hilo.